Habari MsetoSiasa

Moi alizingatia uaminifu kuliko kiwango cha elimu

February 12th, 2020 2 min read

Na JOSEPH WANGUI

RAIS Mstaafu Daniel arap Moi alizingatia zaidi uaminifu kwake wakati alipoajiri maafisa wakuu wa usalama, Kamishna Mstaafu wa Polisi, Bw Duncan Wachira amesema.

Kulingana na Bw Wachira, ijapokuwa Mzee Moi alithamini kiwango cha masomo kwa watumishi wa umma, alizingatia pia bidii, nidhamu na uaminifu kwa utawala wake.

Huku akimtaja marehemu Moi kama mtu aliyekuwa mwenye huruma, Bw Wachira alisema Mzee Moi alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa rais aliyemfuata, Mwai Kibaki na wagombeaji wengine wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanywa mwaka wa 1997.

Katika uchaguzi huo, Bw KIbaki aliibuka nafasi ya pili kupitia Chama cha Democratic Party, akifuatwa na Raila Odinga (National Development Party), Kijana Wamalwa (Ford Kenya), Charity Ngilu (Social Democratic Party) na Martin Shikuku (Ford Asili) miongoni mwa wengine.

Kutokana na taharuki ya kisiasa iliyokuwepo, Moi alimwagiza Bw Wachira kuwapa usalama washindani wake wa urais ili kuhakikisha hawatashambuliwa wala kujeruhiwa kwa njia yoyote wakati wa kampeni.

Wote walipewa walinzi waliojichagulia wenyewe, lakini waliidhinishwa na Bw Wachira.Alizidi kusema, wakati Moi alipochagua wakuu wa polisi, aliwakagua mwenyewe na kuzingatia uaminifu wao kwa serikali yake na uzalendo kwa taifa.

Bw Wachira alikumbuka jinsi Mzee Moi alivyomchagua kuwa mkuu wa idara ya polisi katika mwaka wa 1996 baada ya kuwa mwandani wake kwa karibu miaka 15.

‘Nilikutana na Moi kwa mara ya kwanza nilipokuwa OCPD Nakuru na nilikuwa nasimamia msafara wake karibu kila wikendi kutoka Ikulu ya Nakuru hadi Ikulu ya Nairobi.

Ilikuwa ni kazi ngumu kwa sababu ya ukungu na magari yalihitajika kuendeshwa kwa kasi,’ akasema katika mahojiano nyumbani kwake Hurlingham, nairobi.

Alieleza kuwa, Moi alifahamu kila kitu kuhusu maafisa wa polisi ikiwemo mahali walipokuwa kila wakati, kufuatia jaribio la mapinduzi ya serikali mwaka wa 1982.

Bw Wachira ambaye alifahamika pia kama Bw Strong Man alihudumia taifa kama kamishna wa polisi kwa miaka mitatu kuanzia 1996 hadi 1998.Awali alikuwa mkuu wa polisi katika mkoa, alipohudumu katika mikoa tofauti miaka iliyotangulia.

‘Alinipandisha cheo katika kikosi hadi nikawa kamishna wa polisi,’ akasema Bw Wachira.

Hata hivyo, hali hiyo ya kumpandisha cheo haikupokewa vyema na baadhi ya watumishi serikalini ikabidi wakati mmoja ahamishwe hadi katika Wizara ya Turadhi kuhudumu kama naibu katibu.

Alifanya kazi katika wizara hiyo kwa wiki moja ndipo Moi akagundua, kisha uhamisho huo ukabatilishwa mara moja akarudishwa katika idara ya polisi.

‘Nilivyopandishwa cheo na kuhamishwa mara kwa mara katika maeneo tofauti ya nchi kusimamia vikosi vya usalama ilionekaan na wengine kama kwamba nilikuwa napendelewa,’ akaongeza.Kuna wakati alihamishwa hadi mkoa uliokuwepo wa Pwani kuchukua mahali pa Francis Serem ambaye alikuwa jamaa wa Moi.