HabariSiasa

Moi amshangaa Ruto kuanza kampeni za 2022

May 13th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Baringo Gideon Moi amemshambulia Naibu Rais William Ruto kwa kile anachodai ni hatua ya kughairi Ajenda Nne Kuu za Serikali kwa kuendeleza kampeni za kurithi kiti cha urais 2022.

Bila kumtaja Dkt Ruto kwa jina, Seneta Moi alisema inasikitisha kuwa wanasiasa wengine wameanza kampeni za mapema za urais huku wakiwatelekeza Wakenya waathiriwa wa njaa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Akiongea alipoongoza shughuli ya kuchanga fedha katika kanisa la Runugone Methodist, mwenyekiti huyo wa Kanu alisema huu ni wakati wa kuwahudumia Wakenya na kwamba “nitatangaza mipango yangu ya kisiasa wakati ufaao lakini sio sasa.”

“Sitaki kuanza mjadala wa kinyang’anyiro cha urais wakati huu wanavyofanya watu wengine wenye tamaa. Naomba viongozi wote, akiwemo yule ambaye ameanza kampeni za mapema huku akisahau kumsaidia Rais Kenyatta kuteleza ajenda nne kuu za maendeleo,” akasema Seneta Moi.

“Wakati huo ukitimu, tutaondoa koti zetu zote na kujitosa kwenye uwanja wa vita. Lakini sasa hatufai kujishughulisha na siasa. Tumsaidie Rais kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya,” akaongeza.

Seneta huyo  alikuwa ameandamana na wabunge Gladys Wanga (Homa Bay), Maina Kamanda (Mbunge Maalum) kati ya wengine alisema ana imani kuwa jamii ya Wameru watamuunga mkono “wakati ufaao”.

Dkt Ruto na Seneta Moi ni mahasidi wa kisiasa na wamekuwa waking’ang’ania ubabe katika eneo la Rift Valley.

Naibu Rais anahisi kuwa Gideon Moi anapaswa kuunga mkono azma yake ya urais kwa sababu “niko karibu sana na taji hilo” huku akihisi kuwa hatua yoyote ya kumuunga mkono kiongozi yeyote sharti ielekezwe na haja ya kuwanufaisha Wakenya wote wala sio watu binafsi.