HabariSiasa

Moi asafirishwa Israeli kwa matibabu ya dharura

March 12th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU na WYCLIFF KIPSANG

RAIS Mstaafu Daniel Moi Jumapili alisafirishwa nchini Israeli kupata matibabu ya dharura. Ripoti kutoka kwa familia yake zilisema kwamba Mzee Moi alisafirishwa mjini Tel Aviv kupokea matibabu katika goti lake ambalo limekuwa likimsumbua.

Kwenye taarifa fupi, Seneta Gideon Moi wa Baringo, ambaye pia ni mwanawe, alithibitisha hayo, akiwaomba Wakenya kumwombea babake kupata nafuu haraka.

“Mzee Moi hahisi vizuri. Anatarajiwa kupokea matibabu. Tunamrai mumwombee,” akasema Bw Moi. Afisi ya kiongozi huyo wa zamani ilisema kwamba ameandamana na mwanawe Gideon na daktari wake Dkt David Silverstein.

Dkt Silverstein alisema kwamba wanalenga kupata maoni zaidi ya madaktari kuhusu hali ya goti la Bw Moi. Baada ya matibabu hayo, Mzee Moi amepangiwa kuzuru maeneo ya kihistoria jijini Jerusalem kabla ya kurejea nchini.

Mzee Moi alionekana mara ya mwisho hadharani mnamo Oktoba 26, 2017 akipiga kura yake katika Chuo Kikuu cha Kabarak wakati wa Uchaguzi wa Pili wa urais. Lakini kinyume na chaguzi za hapo awali, alipigia kura katika gari lake.

Mzee Moi amekuwa akiendesha maisha yake kimya kimya katika makazi ya Kabarak, ambapo amekuwa akipokea jumbe mbalimbali, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na mamake, Mama Ngina Kenyatta.

 

Upasuaji mdogo

Mnamo Januari, 27, 2017 Mzee Moi alifanyiwa upasuaji mdogo katika goti hilo katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Matatizo ya goti hilo yalianza mnamo 2006, baada yake kupata ajali wakati akisafiria gari lake aina ya Range Rover lililogongana na gari jingine katika eneo la Rukuma View Point, Limuru.

Mzee Moi alihudumu akiwa rais wa Kenya kwa miaka 24 kati ya 1978 na 2002.

Alichukua uongozi kutoka kwa rais wa kwanza, Mzee Jomo Kenyatta, baada yake kufariki Agosti 22, 1978.

Wakati wa utawala wake, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia umoja na amani nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wa kidemokrasia walimkosoa vikali kwa kuendeleza udikteta, hasa kwa kusisitiza kuwa Kanu ndicho kilikuwa chama pekee cha kisiasa.

Shinikizo hizo ndizo zilimsukuma kuruhusu uwepo wa vyama vingi nchini mnamo 1991, baada ya kuondolewa kwa kipengele 2(a) cha katiba.

Mzee Moi aling’atuka uongozini mnamo 2002 baada ya Kanu kushindwa vibaya kwenye kinyang’anyiro cha urais na muungano wa Narc, ulioongozwa na Rais Mstaafu, Mwai Kibaki.