Habari Mseto

Moi Dei kuadhimishwa

October 9th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba siku ya Alhamisi, Oktoba 10, 2019, ni Sikukuu ya Kitaifa kuadhimisha Moi Dei.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumanne jioni, Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i alisema kuambatana na uamuzi wa mahakama, serikali imeamua kuirejesha sikukuu hiyo na akatangaza kuwa itaadhimishwa kama zamani.

“Kulingana na hitaji la Sheria kuhusu Sikukuu (Sura ya 110, Sheria za Kenya) na uamuzi wa mahakama katika Kesi ya Kikatiba Nambari 292 ya 2017, ninatangaza kuwa Oktoba 10, 2019, itakuwa sikukuu ya kitaifa,” akasema.

Sikukuu ya Moi Dei iliondolewa kutoka kwa orodha ya sikukuu za kitaifa kufuatia kuzinduliwa rasmi kwa Katiba ya Mwaka 2010.

Akitoa uamuzi huo mnamo Novemba 2017 Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga alisema kufutiliwa kwa sikukuu hiyo kulikiuka Sheria kuhusu Sikukuu za Kitaifa.