Habari MsetoSiasa

MOI DEI: Rungu ya Nyayo ilipoanguka na kuvunjika

October 10th, 2018 2 min read

NA WYCLIFFE MUIA

RAIS mstaafu Daniel arap Moi, na mtangulizi wake Mzee Jomo Kenyatta, walikuwa na vifaa maalum vya kuonyesha mamlaka ambavyo walikuwa wakibeba kila mahali.

Mzee Kenyatta alikuwa na usinga, naye Mzee Moi, alikuwa na rungu, almaarufu Fimbo ya Nyayo.

Umuhimu wa Fimbo ya Nyayo haukufahamika vyema na walio kuwa karibu na Mzee Moi hadi mnamo 1981 wakati rungu hiyo iliyokuwa imetengenezwa kwa pembe za ndovu ilipoanguka na kuvunjika.

Kisa hicho kilitokea wakati Mzee Moi alipokuwa ziarani Los Angeles, Amerika baada ya kuhudhuria Kongamano la Umoja wa Matifa mjini New York.

Kuvunjika kwa rungu hiyo kulizua hofu kubwa kwa wasaidizi wa Mzee Moi kwani aliagiza kutengenezewa fimbp nyingine kabla ya kuanza kwa kikao kingine cha marais wa Mataifa ya Dola (Chogm) mjini Melbourne, Australia na kusema hataki kuenekana hadharani bila fimbo hiyo.

Akiongea katika kipindi cha Jeff Koinange Live(KJL), Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya habari za rais huyo mstaafu, Lee Njiru, alisema Mzee Moi alisitisha shughuli zote akiwa Amerika hadi atafutiwe rungu nyingine.

Bw Njiru alisema simu zilipigwa katika Ikulu ya Nairobi na kwa upesi mipango ya kuundwa kwa rungu ingine ikafanywa ili kusafirishwa hadi Australia kabla ya Mzee Moi kuwasili kutoka Amerika.

Kwa mujibu wa Njiru, mmoja wa afisa wa Ikulu ya Nairobi Peter Rotich aliagizwa kuwasilisha rungu mpya kutoka Nairobi, akitumia ndege tofauti kupitia Afrika Kusini, bara Asia hadi akafika Australia.

“Tulikuwa tukielekea Australia kuhudhuria kongamano la Marais kutoka mataifa ya Dola. Ilibidi tutue mjini Honolulu,jimbo la Hawai kwa sababu simu zilipigwa Nairobi, na tukapata afisa wa Ikulu kwa jina Peter Rotich. Afisa huyo aliamrishwa kuwasilisha rungu mbili za pembe ya ndovu kutoka Nairobi hadi Australia kabla tuwasili,”alisema Njiru.

Ilikuwa lazima Rotich awasili kabla ya Moi kutia Australia, kwa sababu Mzee Moi alikuwa anataka kusalimia watu akiwa na rungu yake baada ya kuwasili kama kawaida yake.

Inaripotiwa kuwa Rotich alifika Australia kwa saa aliyotarajiwa na kuingia kwa ndege ya Moi kabla atoke ili ampe rungu mpya.

Mzee Moi baadaye alishuka kwa ndege akiinua rungu yake bila hata kujua iwapo kulikuwa na tofauti ya rungu aliyokuwa nayo mbeleni.

Njiru alisema kisa hicho kilimdhihirishia maana kamili ya kuwa mamlakani kwani rungu tu ilisababisha kusitishwa kwa shughuli muhimu huku ikisafirishwa kwa ndege kadhaa kutoka Nairobi hadi Australia.