Habari

MOI DEI YA MAUTI: Watu 55 waangamia ajalini

October 10th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

JUMLA ya watu 55 walithibitishwa kufa, wakati basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali mbaya, eneo la Tunnel, Kericho katika barabara ya Londiani-Muhoroni, Moi Dei alfajiri.

Watu 12 waliojeruhiwa katika ajali hiyo ya alfajiri walikimbizwa hospitalini, wengine wakiwa na majerahja mabaya.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kericho James Mugera alithibitisha ajali hiyo, akisema wanaume 31, wanawake 12 na watoto saba waliangamia katika ajali hiyo ya kusikitisha.

Bw Mugera alisema kuwa basi hilo linamilikiwa na kampuni ya Western Cross Express, lakini jina lake ni Home Boyz.

Vilevile, mkuu wa trafiki kanda ya Bonde la Ufa Ziro Arome aliongeza kuwa majeruhi walikimbizwa katika hospitali za Muhoroni na ya wilaya ya Kericho.

Wakazi wa eneo ilikotokea ajali walijitokeza mapema kujaribu kuokoa manusura, huku wingu la simanzi likitawala eneo hilo.

Basi hilo la abiria 67 lilikuwa likielekea maeneo ya Magharibi mwa nchi kutoka Nairobi wakati lilipoteza mwelekeo na kuanguka katika eneo lililoenda chini kando mwa barabara, katika shamba la mtu.

Bw Mugera alisema kuwa idadi ya walioaga ingetarajiwa kupanda kwa kuwa wengine bado walikuwa wamebanwa katika vifusi vya gari hilo.