Habari

Moi kupewa mazishi ya taadhima kuu

February 4th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa zamani Daniel Arap Moi huku akiamuru bendera za kitaifa zipeperushwe nusu mlingoti kote nchini kuanzia leo Jumanne.

Kwenye taarifa rasmi kwa umma kuhusu kifo cha Rais huyo wa pili wa Kenya, Rais Kenyatta amesema kipindi hicho cha maombolezo kitadumu hadi siku ambapo Mzee Moi atazikwa.

Na Rais huyo mstaafu atapewa mazishi ya kitaifa yakiandamanishwa na heshima na taadhima zote za kijeshi, Rais Kenyatta akaongeza.

“Chini ya mamlaka niliyopewa kama Rais wa Jumhuri wa Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, naamuru kwamba kwa heshima ya kumbukumbu ya Marehemu Daniel Toroitich Arap Moi, natangaza kipindi cha maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo (Jumanne) hadi wakati wa mazishi yake,” akasema kwenye taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyumba vya habari.

Akaongeza: “Marehemu Daniel Toroitich Arap Moi atapewa Mazishi ya Kitaifa huku Heshima zote za Kiraia na Kijeshi zikitolewa.”

Awali, Rais Kenyatta alitangaza rasmi kifo cha Moi kilichotokea katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha miezi minne.

“Ni kwa huzuni kuu, natangaza kifo cha Kiongozi Mkuu Afrika Mheshimiwa Daniel Toroitich Arap Moi, Rais wa Pili wa Jamhuri ya Kenya. Rais huyo wa zamani alifariki katika Nairobi Hospital asubuhi mnamo Februari 4, 2020, akiwa na familia yake,” Rais Kenyatta akasema kwenye taarifa.

“Sifa zake zinadumu nchini hadi siku ya leo (Jumanne), zikidhihirishwa ndani ya Filosofia ya Nyayo ya ‘Amani, Upendo na Umoja’ ambayo ilikuwa kaulimbiu yake alipihudumu kama Rais wetu.”

Katika hotuba fupi nje ya Nairobi Hospital Jumanne asubuhi mwanawe Seneta Gideon Moi alisema babake alifariki kwa utulivu.

Alisema familia inawashukuru kwa kumwombea Rais mstaafu alipokuwa amelazwa hospitalini humo akipokea matibabu.

“Nilikuwa kando yake, na kama familia tumekubali. Langu ni kutoa shukrani zangu kwa Wakenya wote kwa kuombea Mzee na familia yetu. Asanteni nyote,” amesema

Mwili wa Mzee Moi umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee, Nairobi.