MakalaSiasa

DANIEL MOI: Twiga aliyeweza kuona mbali

March 24th, 2019 4 min read

NA KENYA YEARBOOK

DANIEL Toroitich arap Moi, alizaliwa Septemba 2, 1924, katika kijiji cha Kurieng’wo, Sacho, wilayani Baringo. Alikuwa mwana wa tano wa mke wa kwanza wa baba yake.

Moi alipatiwa jina Toroitich, linalomaanisha “karibisha mifugo nyumbani,” ishara ya jukumu muhimu ambalo mifugo hutekeleza katika utamaduni wake.

Babake Moi alikufa wakati yeye (Moi) alikuwa na umri wa miaka minne na kaka yake, Tuitoek, akawa mlezi. Ni Tuitoek aliyemshawishi Moi kwenda shule akiwa na umri mdogo ili aweze kujiepusha umaskini na dhuluma za kikoloni.

Mnamo 1934, Moi alianza masomo katika shule ya Africa Inland Mission, Kabartonjo, takriban kilomita 45 kutoka nyumbani kwao.

Mnamo Oktoba 20, 1936, alibatizwa na kuitwa Daniel. Mnamo 1938, alihamishiwa shule ya African Inland Mission, Kapsabet na baadaye shule ya African School Kapsabet, ambapo alikuwa kiranja mkuu na nahodha wa timu ya soka. Alifanya kazi za vibarua akiwa shuleni na nje ya shule ili aweze kukimu mahitaji yake ya kimsingi.

Mnamo 1945, Moi alichaguliwa kujiunga na shule ya upili ya Alliance lakini, kwa masikitiko, serikali ya kikoloni haikumruhusu. Badala yake, alitumwa chuo cha mafunzo ya ualimu.

Maswali yamekuwa yakiulizwa: Kwa nini serikali ya kikoloni ilimnyima Moi nafasi muhimu ya kusomea Alliance? Ni nini walikuwa wameona ndani yake?

Alipomaliza mafunzo ya ualimu, alitumwa Kabarnet kama mwalimu mkuu.

Alisoma binafsi na kufuzu mtihani wa London Matriculation Examinations. Mnamo 1949, alipandishwa cheo na kuwa mwalimu wa kiwango cha P2 baada ya kozi fupi katika chuo cha Kagumo.

Alihamishwa hadi Tambach Government African School kama mwalimu wa walimu. Moi alimuoa Helena (Lena) Bomet mwaka wa 1950 na wamejaliwa watoto wanane- mabinti watatu na wavulana watano.

Mnamo 1950 alihudhuria mafunzo katika Jeans School (sasa inajulikana Kenya Institute of Administration) na baadaye akatumwa kufanya kazi Government African School, Kabarnet, ambako alifunza hadi 1955 alipojiunga na siasa.

Kujiunga na siasa kwa Moi, kulifuatia mkutano aliofanya na kundi la wapiganaji wa uhuru chini ya uongozi wa Brigedia Daniel Njuguna aliyemtembelea Juni, 1955.

Aliunga vita vyao na baada ya kuwalisha na kuwakinga kwa wiki mbili, aliwapatia chakula na Sh500.

Mnamo Oktoba 1955, Moi alichaguliwa kutoka orodha ya watu wanane walioteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Joseph ole Tameno, ambaye alikuwa amejiuzulu kutoka kiti kisichokuwa rasmi katika Legco.

Moi alipoketi Legco akiwa na wanachama wengine wanne pekee Waafrika mnamo Oktoba 18, 1955, hakujua yaliyokuwa yakimsubiri.

Yeye, hata hivyo, alikabiliana na changamoto mpya na, mnamo 1956, aliwasilisha mswada kutaka walimu Waafrika, waruhusiwe kuunda chama chao wenyewe.

Chama cha Kitaifa cha Muungano wa Walimu Kenya (Knut) kiliundwa na kusajiliwa was 1957.

Alishirikiana na viongozi wengine kama vile Eliud Mathu, Ronald Ngala na Masinde Muliro, kutetea Jomo Kenyatta kuachiliwa kutoka kizuizini na idadi ya Waafrika katika Legco kuongezwa.

Mnamo 1959, aliongoza kundi la viongozi kumtembelea Kenyatta kizuizini Lodwar.

Mnamo 1960, Moi na wanachama wengine Waafrika katika Legco, walishiriki katika mazungumzo ya kikatiba katika Lancaster House jijini London katika maandalizi ya Uhuru wa Kenya kutoka kwa Uingereza.

Waliporudi nchini, walinuia kuanzisha chama kimoja cha kitaifa cha kisiasa. Lakini tofauti kati yao zilifanya waunde vyama viwili- Kanu cha Gichuru, Odinga na Mboya kilichobuniwa Kiambu, na Kadu cha Ngala (rais), Moi (mwenyekiti), Muliro (naibu- mwenyekiti) na Martin Shikuku (katibu- mkuu) walichounda wakiwa Ngong.

Moi na wengine katika Kadu, ambao walitoka jamii ndogo, walikataa Kanu wakidai ilikuwa ikiwakilisha maslahi ya jamii kubwa, Waluo na Wakikuyu. Kwa hivyo, waliamua kuunda muungano wa makabila mengi.

Kwenye uchaguzi wa 1961, Kanu ilishinda viti 19 na Kadu kikapata 11. Lakini Kanu ilikataa kuunda serikali hadi Kenyatta aachiliwe huru.

Lakini Kadu ilikubali na Moi akateuliwa Katibu wa Bunge (waziri msaidizi) katika Wizara ya Elimu mnamo 1961. Baadaye alihudumu katika wizara za Elimu na Serikali za Wilaya.

Katika uchaguzi wa 1963 ambao ulileta uhuru, Kadu ilikataa kuwasilisha wagombeaji kupinga Kanu, kilichokuwa wakati huo chini ya uongozi wa Kenyatta baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini 1961. Kadu kilishindwa na kuwa katika Upinzani. Kenyatta alichaguliwa Waziri Mkuu.

Akiwa mwenyekiti wa Kadu, Moi aliona utata wa siasa na akaamua kukumbatia umoja wa kitaifa. Hii ndiyo ilifanya Kadu kuvunjwa Novemba, 1964. Wanachama walijiunga na Kanu na Kenya ikawa taifa la chama kimoja, japo sio kisheria.

Kenyatta alimteua Moi Waziri wa Mashauri ya Ndani, wadhifa ambao alihifadhi hata alipokuwa Makamu- Rais. Mashauri ya Ndani ulikuwa wadhifa muhimu kwa sababu alikuwa akisimamia magereza, polisi na Idara ya Uhamiaji.

Toleo la Africa Confidential la Juni, 1990, lilisema kuhusu Moi na Wizara ya Mashauri ya Ndani: “Alifanya urafiki ambao ulimfaa miaka ya baadaye. Jukumu lake la kutoa paspoti lilimkutanisha na wafanyabiashara kutoka bara Asia na makampuni kutoka Uingereza. Lilikuwa jukumu la Moi pia, kuteua wakuu wa polisi, magereza na huduma za uhamiaji. Hii ilimfaidi miaka ya baadaye wakati huduma ya polisi ilikuwa imejaa watu ambao Moi aliteua.”

Lakini kumezwa kwa Kadu hakukutuliza siasa. Badala yake, kulizua vita chungu nzima katika Kanu asilia, kati ya mirengo miwili, mmoja ukimuunga Rais Kenyatta na mwingine Makamu- Rais Odinga.

Kufikia 1966, tofauti zilikuwa zimefikia kiwango ambacho hazingetatuliwa na wakati Odinga alipovuliwa wadhifa wa naibu- rais katika kongamano la Limuru, alijiuzulu kutoka chama hicho na kuunda KPU.

Joseph Murumbi, aliyekuwa Waziri, aliteuliwa Makamu- Rais. Lakini hakuhudumu kwa mwaka.

Mnamo Januari, 1967, Kenyatta alimteua Moi, 43 Makamu- Rais kufuatia kujiuzulu kwa Murumbi. Wadadisi wa kisiasa wanasema Moi aliteuliwa kwa sababu anatoka kabila ndogo katika Kenya iliyogawanyika kikabila.

Ilisemekana hakuwa na ngome thabiti ya kisiasa na hakuwa mshirika katika muungano wa Wakikuyu na Waluo wa miaka ya sitini.

Kama Makamu wa Rais, Moi alichukuliwa kuwa asiyekuwa na mambo mengi. Lakini kama Odinga alivyosema katika kitabu chake alichochapisha 1967, Not yet Uhuru, Moi alikuwa kama “twiga mwenye shingo ndefu anayeona mbali.”

Aliepuka dhoruba nyingi ikiwa ni pamoja na shinikizo za kubadilisha katiba ili Makamu wa rais asiweze kutwaa mamlaka mara moja kwa muda wa siku 90 kiti cha Rais kikibaki wazi. Alihudumu kama Makamu Rais chini ya Kenyatta kwa miaka 11 tangu 1967.

Kenyatta alipokufa Agosti 22 1978, Moi alitwaa urais kwa ruhusa ya chama cha Kanu na usaidizi wa viongozi wa Akikuyu kama Waziri wa Fedha Mwai Kibaki na Mkuu wa Sheria Charles Njonjo. Moi alimteua Kibaki kuwa makamu wake wa rais.

Moi alisisitiza kuwa angeendeleza sera za Kenyatta katika kauli mbiu yake ya Nyayo au “ kufuata nyayo za hayati rais.” Kitu cha kwanza ambacho Moi alifanya, ilikuwa ni kuzuru kote nchini na kukutana na jamii zote.

Pia, alianzisha maziwa ya bure kwa wanafunzi wote wa shule za msingi, akaachilia wafungwa wa kisiasa na kufunga kampuni za kununua mashamba ambazo zilikuwa zimetumia vibaya wamiliki wa mashamba madogo kwa miongo mingi.

Moi alitawala nchi kwa miaka 24 na kumpokeza Kibaki utawala mnamo Desemba, 2002, Uchaguzi Mkuu ambao Kanu iliondolewa mamlakani baada ya miaka 39 na Muungano wa National Alliance Rainbow Coalition (Narc).

Moi alimkabidhi Kibaki mamlaka katika sherehe iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu kuwahi kuonekana Nairobi.

Huo ulikuwa mwisho wa maisha ya kisiasa ya miaka 47 ya Moi, alikuwa ameshinda kila uchaguzi kama mbunge wa Baringo ya Kati na kama Rais wakati wa enzi za utawala wa chama kimoja. Alichaguliwa bila kupingwa 1979, 1983 na 1988. Alishinda tena 1992 na 1997.

Kwa wakati huu Moi amestaafu. Lakini mara kwa mara huwa anakosoa serikali na wapinzani wake wa kisiasa.