Moise Kean afungia PSG tena na kuwaongoza kutua kileleni mwa Ligue 1

Moise Kean afungia PSG tena na kuwaongoza kutua kileleni mwa Ligue 1

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) waliwacharaza Nice 2-1 uwanjani Parc des Princes, Februari 13, 2021, na kutua kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Julian Draxler aliwaweka PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligue 1 uongozini kunako dakika ya 22 kutokana na kombora lililovurumishwa na Mauro Icardi kabla ya kugonga mhimili wa goli na mpira kumrudia Draxler.

Rony Lopes alifungia Nice bao la kusawazisha katika dakika ya 50 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya beki Marquinhos Correa.

Nusura Amine Gouiri awafungie Nice bao la pili katika dakika ya 60 ila fataki yake ikabusu mwamba wa lango la PSG.

Mshambuliaji Moise Kean anayechezea PSG kwa mkopo kutoka Everton alivunia kikosi cha kocha Mauricio Pochettino alama zote tatu katika mechi hiyo kwa kufunga bao la pili na la ushindi kwa upande wa PSG katika dakika ya 76.

PSG waliokuwa wakichezea nyumbani, walivalia jezi yao mpya ya mseto wa rangi ya zambarau na zambarau nyeupe. Baada ya ushindi huo, miamba hao wa soka ya Ufaransa na wanafainali wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20, sasa wanajivunia alama 54 sawa na Lille ambao wana mechi moja zaidi ya kusakata ili kufikia michuano 25 ambayo tayari imepigwa na PSG.

Kwingineko, Olympique Lyon walipoteza nafasi ya kutua kileleni mwa jedwalini la Ligue 1 mnamo Jumamosi baada ya kupigwa 2-1 na Montpellier. Lyon kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 52 huku pengo la pointi 17 likitamalaki kati yao na nambari nane Montpellier.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Februari 13):

PSG 2-1 Nice

Reims 1-1 Lens

Lyon 1-1 Montpellier

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Dereva Chager kutumia mashindano ya Autocross Kasarani...

EPRA: Atwoli aitaka wizara husika ajitokeze kumtetea raia...