Michezo

MOKAYA: Bado Guardiola ni mkali kuliko Mourinho

November 19th, 2018 2 min read

NA JOB MOKAYA

Juma lililopita kocha wa Manchester United Jose Mourinho alinyolewa upara bila maji na kocha wa Manchester City baada ya United kulimwa mabao 3-1 kwenye mechi iliyopigwa katika uga wa Etihad.

Ingawa wengi walitarajia kwamba Manchester United ingepokea kichapo mbele ya City, kuna wale mashabiki wa Manchester United waliotarajia kwamba City ingelala.

Hata hivyo, nao hawakushangaa sana kutokana na matokeo hayo. Lililodhihirika sana ni ufa mkubwa ulioko kati ya timu hizi mbili huku Manchester City ikionesha kupiga hatua nyingi sana mbele ya United.

City ilimiliki mpira na kupenya kwa urahisi huku United ikionekana kutapatapa hapa na pale bila mpangilio wowote. Ilikuwa dhahiri kama mchana wa jua kwamba Pep alimzidi maarifa Mourinho, na vijana wake Pep walikuwa katika ulimwengu wa mawinguni huku wake Mourinho waking’ang’ana papa hapa duniani.

Licha ya yote hayo, Jose Mourinho anaonekana kuwa kocha mzuri na mwenye mbinu nzuri za ufundishaji ukilinganisha na Pep. Ingawa Manchester United ilibwagwa na Manchester City, kiuwezo, bado Mourinho yuko hatua nyingi sana mbele ya Guardiola kiufundi.

Kwa sasa, kile kinachomfanya Gaurdiola aonekane kumzidi Mourihno maarifa ni kwamba wachezaji wake wanatambaa kwa urahisi na kuupiga mpira hapa na pale kwa wepesi nao Manchester United wakionekana kuhitaji miwani ili kuona uliko mpira.

Karibu kikosi kizima cha Manchester City kina wachezaji wapya pekee tena wenye kucheza vizuri sana. Ni mastaa walionunuliwa kutoka klabu tofauti ambako walikuwa waking’aa sana.

Kabla ya kuwaleta wachezaji hawa, Pep alikumbana na msimu mgumu sana miaka miwili iliyopita hata akaishia kumaliza katika nafasi ya nne pekee. Hata hivyo, aliwaachilia wachezaji karibu wote waliokuwako kwenye timu na kuleta wengine.

Wachezaji waliobaki City baada ya kuingia Pep kwa sasa ni wawili watatu hivi. Wengine wote kuanzia mlindalango, nambari mbili, nambari tatu, nne, tano, sita, saba, nane na kadhalika ni wageni. Wale wachache waliobaki kama Aguero pia walikuwa wapigwe mnada ila kuimarika kwao kumewasaidia.

Kwa upande wao, Manchester United wana kikosi hafifu sana isipokuwa kwa wachezaji wawili watatu hivi.

Yaani kinyume kabisa cha Manchester City. Wachezaji hao wawili watatu hivi wa Manchester United ni golikipa mwenyewe David de Gea, Paul Pogba, labda Marcus Rashford, labda Anthony Martial na labda Romelu Lukaku.

Wengine wote karibu kikosi kizima cha ulinzi ni maziwa lala au mgando. Maguu yao yameganda tu. Maziwa lala ni Ashley Young kikongwe mwenye miaka 34, Antonio Valencia kikongwe mwingine mwenye miaka 34, Chris Smalling, Phil Jones na Marcus Rojo. Sitamwacha nje Erick Bailey.

Wakati una safu nzima ya ulinzi ambayo ni maziwa lala hata wewe utalala pia. Kwa hivyo, uzuri wa Pep hauko kwenye Pep mwenyewe bali kwenye wachezaji wake ambao wote ni wa haiba ya juu. Nao ubaya wa Mourinho uko kwenye wachezaji wake maziwa lala.

Mtindo wa usakataji soka wa Pep, yaani tiki-taka unawafanya wachezaji kushirikiana zaidi , hivyo ni rahisi kununua mchezaji yeyote.

Mtindo wa Mourinho wa kila mchezaji kucheza kwa nguvu zote unawafanya wachezaji wazuri kumkataa Mourinho.