Michezo

MOKAYA: Ole Gunnar na Mourinho hawana tofauti

April 15th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

BAADA ya kupigwa kwa mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) kati ya Manchester United na Barcelona, wachanganuzi wengi wa soka waliamini kuwa kwa yakini hakuna tofauti ya uchezaji kati ya kocha wa zamani wa Man-United Jose Mourinho na kocha wa sasa Ole Gunnar Solskjaer.

Naye kocha mwingine wa wa zamani wa Man-United Louis van Gaal alidokeza kwamba mfumo wa usakataji soka wa Ole Gunnar ni uleule wa kujihami na kuishauri timu kuvizia namna alivyokuwa anafanya Mourinho huku tofauti tu ikiwa kwamba Ole Gunnar alipata matokeo mema zaidi ya Mourinho.

Solskjaer ameshinda mechi 16 kati ya mechi 20 akiwa kocha wa Man-United ila Van Gaal anasisitiza kuwa Solskjaer hajaleta mabadiliko yoyote timuni na habari zozote kama hizo ni uvumi, na siku hizi uvumi ndio hutawala soka.

“Watu wanadhani kwamba habari za uvumi zilianza tu wakati Donald Trump alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Katika soka, uvumi wa soka kama huu kwamba Solskjaer ameibadili Man-United zimekuwepo kwa miongo mitano sasa,” Van Gaal aliambia jukwaa la spoti la BBC.

Kulingana na Van Gaal, timu ya Man-United iliacha kushambulia wakati Mourinho alipokezwa majukumu ya kuiongoza na baada ya yeye kuondoka, hamna mabadiliko yoyote yaliyoletwa na Ole Gunnar pasi na ushindi wa hapa na pale ila mfumo wa usakataji soka ni ule ule tu.

“Mourinho alibadili mfumo wangu wa ushambuliaji na kuegesha basi mbele ya mlango kisha kushambulia kwa kuvizia. Na sasa kuna mwingine ambaye anaegesha basi mbele ya mlango na kucheza mpira kwa kuvizia yaani kushtukiza. Tofauti kuu ya Mourinho na Solskjaer ni kwamba Solskjaer anapata ushindi mwingi,” Van Gaal alifafanua.

“Mimi sipo huko sasa hivi ila nitasema kuwa mazingira ya mashabiki ni mazuri zaidi ndani ya uwanja ukilinganisha na ilivyokuwa kwa Mourinho. Ni sahihi pia kusema kwamba Pogba ameimarika chini ya Solskjaer kwani anapewa nafasi ya kucheza sehemu anayopendelea.

“Man-United hawachezi vizuri, hawashambulii, hawachezi namna Sir Alex Ferguson alivyokuwa akichezesha kikosi. Wanajihami, wanacheza kwa kuvizia. Ukiipenda kauli yangu, utaipenda, ukidhani Man-United wanacheza vizuri, sawa, hilo ni juu yako. Ila, ukweli wangu ni kuwa hawachezi vizuri,” Van Gal alisema.

Huenda madai ya Louis van Gaal yana ukweli ukiichambua mechi za juma lililopita ambapo Man-United ilishindwa kwa bao moja kwa nunge dhidi ya Barcelona huku ikishindwa kupiga shuti yoyote kuelekea langoni pa wenyeji wao.

Man-United ilipofungwa bao kunako dakika ya 13, umiliki wa mchezo ulikuwa asilimia 90 kwa Barcelona na asilimia 10 kwa vijana wa Ole Gunnar huku wachezaji wa Man-United wakiwa wameegesha basi.Walitegea kushambulia kutoka nyuma yaani, kucheza mpira wa kushtukiza anavyosema Van Gaal, lakini hilo halikuwezekana.

Aidha, Man-United ilishinda tu mechi moja kati ya mechi tano kwenye mchezo wake wa hivi karibuni ikiwamo mechi dhidi ya Arsenal, Chelsea na Wolverhampton. Ingawa Ole Gunnar alifanya muujiza kule Ufaransa kwa kuishinda Paris Saint-Germain (PSG), inasubiriwa kuonwa kama atafanya muujiza kama huo huko Barcelona kwenye mchezo wa marudiano. Kikosi kizima cha United kinaelekea kumuunga mkono Solskajer ambaye alipewa kandarasi ya kudumu kuiongoza Man-United hivi majuzi.

Hivyo, wachezaji kama vile Paul Pogba na Marcus Rashford wameng’aa sana chini ya Solskjaer.

Muhimu ni kwamba, Solskjaer hana lolote jipya akilinganishwa na Mourinho na iwapo atafaulu,

basi itakuwa ametumwa na Mourinho atumie mbinu zake kushinda mechi. Wakati wa kuzinduka umefika kwa Solskjaer, kwani asipotahadhari, ataanza kupoteza mechi moja baada ya nyingine na punde si punde, atapigwa kalamu!