Michezo

MOKAYA: Zidane amuache Mourinho afanye kazi

September 17th, 2018 2 min read

NA JOB MOKAYA

MSIMU wa Ligi Kuu ya Uingereza umeanza tena kwa kishindo. Kocha Jose Mourinho sasa amekalia kigoda cha Old Trafford. Akikalia kigoda mtii. Ingawa Manchester United haijaanza vyema kampeni hii, ni vyema kwa Mourinho kuheshimiwa.

Huku dirisha la usajili likiwa limefungwa, huenda Mourinho anazidi kukuna kichwa kuhusu kushindwa kupata sajili wa safu ya nyuma aliowataka. Kushindwa kwingi kwa United kumetokana na madifenda kulaza damu uwanjani.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu, Mourinho aliwaambia waandishi wa habari kwamba alihitaji kuwasajili wachezaji wanne wakuu. Madifenda wawili, kiungo wa kati mmoja, na wing’a mmoja.

Kwa mshangao wake, Mourinho hakuweza kupata sajili yeyote na michuano ya awali haijawa mizuri. Ndio maana sasa pana uvumi kwamba Zinedine Zidane ashakata tikiti ya ndege kuja kunyakua kazi yake Mourinho.

Zidane mwenyewe alishinda mataji tisa katika misimu yake mitatu kule Real Madrid, matatu yayo yakiwa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League) akiwa ametinga mara tatu mfululizo akiwa kocha wa kwanza kufanya hivyo.

Ingawa ni rahisi kuafikia uamuzi kwamba Zidane almaarufu Zizou ni kocha mzuri na mwenye haiba ya kufunza timu nyingine kubwa, ukweli ni kwamba Zidane alirithi kikosi imara sana kambini mwa Real.

Kikosi alichorithi Zidane ndicho kilichokuwa bora zaidi Ulaya nzima, kikiwa na wachezaji kama vile Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Gareth Bale, Sergio Ramos, Marcelo, Varane miongoni mwa wengine.

Ilikuwa rahisi kwa kikosi kama hiki kutamba koteUlaya hadi kunyakua Kombe la Klabu Bingwa mara tatu mfululizo. Ingawa katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Zidane alifeli na kumaliza wa tatu.

Endapo matokeo ya Man-United yataendelea kudorora na kusababisha ‘The Special One’ kupigwa kalamu kama alivyofanywa akiwa Chelsea, naye Zidane apawe mikoba ya Mourinho, mambo huenda yakawa magumu sana kinyume na ilivyokuwa Real.

Mwanzo, atapatana na madifenda butu kama vile Matteo Darmain, Phil Jones, Eric Bailly na Chris Smalling. Antonio Valencia na Ashley Young wanaelekea kustaafu hivyo hawatakuwa na mchango mkubwa mbeleni.

Aidha, Zidane atakumbana na kikosi cha ushambulizi chenye Romelu Lukaku, Alexis Sancez, Marcus Rashford na Anthony Martial. Hawa ukilinganisha na kikosi alichokuwa nacho Zidane huko Real, utaona pengo kubwa pale mbele.

Mashambulizi ya Real yaliongozwa na Ronaldo akisaidiwa na Bale, Benzema, James Rodriguez na Alvaro Morata. Hawa, wako mbele sana ya wenzao wa Man-United.

Kibarua kikubwa zaidi kwa Mourinho hivi sasa ni kuhakikisha kuwa anashinda mechi zote za timu ndogondogo kama vile ilivyofanya Manchester City msimu uliopita na hata Chelsea.

Endapo Mourinho atalemewa kabisa na ukufunzi kisha kutimuliwa, Zidane hatakuwa chaguo bora. Ingawa Man-United ina wachezaji wachache wenye kiwango cha kimataifa, wengi ni wenye uwezo wa wastani tu ambao hawatamsaidia kitu Zidane.

Muhimu kwa Zidane ni kumwachia Mourinho hewa ya kupumua. Hata hivyo kwa Mourinho, imekuwa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu uchungu kwani naye alimwandama Louis van Gaal hadi akatimuliwa.