Mombasa Olympic Ladies FC yasajili mastaa 10 kupania kurudi Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake

Mombasa Olympic Ladies FC yasajili mastaa 10 kupania kurudi Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

TIMU ya Mombasa Olympic Ladies FC inajiandaa kuhakikisha inapanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Kenya ya Soka ya Wanawake na kuimarisha kikosi chake kufanikisha nia hiyo, imesajili wachezaji wapya 10.

Kocha wa timu hiyo, Joseph Oyoo amesema wamesajili chipukizi hao 10 kuimarisha kikosi ili waweze kushinda taji la Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza msimu huu. Mombasa Olympic inataka kurudi ligi kuu baada ya kuwa nje kwa misimu minne iliyopita.

“Tumeshakaa ligi ya kitaifa kwa kipindi cha kutosha na sasa tunajitayarisha kurudi ligi kuu ambapo wachezaji wetu wataonekana na wakuu wa benchi la ufundi wa timu ya taifa ya Harambee Starlets na maskauti klabu kubwa za hapa nchini na ng’ambo,” akasema Oyoo.

Wachezaji hao wapya ni Fatma Florence kutoka Voi, Grace Willy (Mikindani), Faithcuster Nyamai (Kitui Starlets), Alice Syambua (Mshale, Kitui), Vivian Adhiambo (St Alfred, Homa Bay), Lilian Mvurya (St John’s Kaloleni), Dorcus Mwaka (Kwale Girls), Happy Muta (St John’s) na Hadija Kiidi (Laikipia).

Oyoo ameambia Taifa Leo Dijitali kuwa wamewapa ruhusa wachezaji kadhaa kujiunga na timu za ligi kuu ili wapate maslahi yao ya kuinua vipaji vyao pamoja na kujisaidia kimaisha wao wenyewe na familia zao.

Wachezaji wa Mombasa Olympic Ladies FC wakifanya mazoezi katika uwanja wa Ziwani Lasco kujitayarisha kwa mechi zao za Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza. PiCHA/ABDULRAHMAN SHERIFF

“Hatuwezi kuwazuia wachezaji wanaotaka kuihama timu bora sababu iwe ya kuendeleza vipawa vya uchezaji wao na maslahi ya maisha yao,” akasema mkufunzi huyo aliyekataa kutaja wale waliohama hadi watakapokamilisha mipango yote ya uhamisho wao.

Lakini tetesi kutoka klabu hiyo zilifahamisha Mwanaspoti kuwa wengi wa wachezaji hao wamesajiliwa na klabu ya Ligi Kuu ya Kenya ya Soka la Wanawake Zetech Sparks ambayo imepania kuhakikisha wanabeba ushindi wa ligi hiyo msimu ujao.

Inaaminika wachezaji wa Mombasa Olympic waliosajiliwa na Zetech Sparks ni Milka Omondi, Cameron, Twaiba Mohamed and Monalisa Anyango hali Melly Anyango amesajiliwa na klabu inayoshiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza ya Soccer Sisters FC baada ya kupata ofa nzuri.

Mnamo miaka kadhaa iliyopita, Mombasa Olympic ilitoa wachezaji wazuri ambao kati yao hivi sasa wanachezea klabu za ligi kuu wakiwemo straika wa timu ya taifa ya Harambee Starlets,  Mwanahalima Adam na Nuru Mustafa ambao wamesajiliwa na Thika Queens FC.

Wachezaji kadhaa waliobakia katika kikosi cha msimu uliopita ni Selina Kahinmdi, Hawa Mwakudu, Fatuma Mpole, Mishi Mbaro, Grace Wekesa, Sharifa Salim, Diana Akinyi, Mercy Sewe, Rael Atieno, Involata Mukosh, Vivian Okinda, Pecky Cynthia, Monica Changawa, Treda Khamete, Jane Ngege, Shantel Muhonja and Hajra Omar.

  • Tags

You can share this post!

Dzeko afunga mabao mawili na kusaidia Inter Milan kupepeta...

Hizi ndizo athari za marufuku kwa wanasiasa madhabahuni