Habari Mseto

Mombasa yawataka wakazi kukoma kuwabagua makahaba na mashoga

June 30th, 2019 2 min read

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya kaunti ya Mombasa imeanza kuwahudumia makahaba, wapenzi wa jinsia moja na huntha (watu wenye sehemu mbili za uzazi) kwa kuwapa huduma za afya ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Afya katika kaunti hiyo, Dkt Shem Patta, amewahimiza wakazi wa Mombasa wawakubali watu hao ambao wamekuwa wakichukuliwa kuwa na tabia zisioambatana na maadili.

“Ni dada na kaka zetu, tunaishi nao katika jamii zetu. Tusiwahukumu manake hili ni swala ambalo limo miongoni mwetu. Tukiwakubali wataanza kwenda katika vituo vya afya kupokea matibabu na hivyo basi tutapunguza maambukizi ya ukimwi,” alisema Dkt Patta.

Kwenye mkutano wa afya katika afisi ya shirika la Msalaba Mwekundu, Dkt Patta alisema wapenzi wa jinsia moja na makahaba yafaa wakubaliwe na jamii zote ili Wakenya washirikiane kupunguza kuenezwa kwa maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi.

Alionya kuwa takwimu zinaonyesha ukimwi miongoni mwa kundi hilo bado ni hatari na endapo juhudi hazitachukuliwa basi huenda maambukizi yakaenea.

Dkt Pata alisema awali, kaunti ya Mombasa, ina idadi kubwa ya watu wanaoishi na ukimwi kwa asilimia 11, zaidi ya ile ya kitaifa ambayo ni asilimia 7.5.

“Lakini mwaka wa 2018 idadi ikaanza kupungua hadi asilimia 4.1 kufuatia mikakati tuliyoweka tukishirikiana na makundi ya kijamii ikiwemo Reachout Trust Centre, Mewa, AIDS Healthcare Foundation (AHF) na shirika la msalaba mwekundu,” alisema Dkt Patta.

Dkt Patta alisema ruwaza ya Mombasa inapania kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari kwa asilimia 75.

Aidha alionya wakazi dhidi ya unyanyapaa akisisitiza kuwa unachangia pakubwa kwa msongo wa mawazo miongoni mwa watu wanaoishi na ukimwi.

“Unyanyapaa ni swala nyeti, jamii inafaa kubadilika. Kama serikali ya kaunti tunapania kuwahamasisha ili kupunguza unyanyapaa kwa asilimia 50. Pia tunataka kupunguza vifo vya ukimwi kwa kuwahamasisha wakenya kwenda kupimwa, wale wanaopatikana na ukimwi wanapewa dawa ili wapate afya na kurefusha maisha yao,” alisema.

Dkt Patta alisema takwimu za idara ya afya zinaonyesha watu elfu 41,000 wanaishi na ukimwi kaunti ya Mombasa, huku ikipata maambukizi mapya 1700 kila mwaka.

Hata hivyo alisema dawa za ARV’s, zinasaidia wale wanaoishi na ukimwi kuishi maisha bora ya afya.

Kuna zaidi ya watu 8,000 ambao ni wapenzi wa jinsia moja huku wale wanaojidunga sindano za dawa za kulevya wakizidi 18,000 nchini, kaunti ya Mombasa ikiwa na idadi kuwa.

Ugonjwa wa HIV na Hepatitis C huenezwa na watu wanaoishi na maradhi hayo wanaotumia sindano moja kujidunga dawa za kulevya.

Mkurugenzi huyo wa afya alisema kuna vituo 18 za afya ambapo wapenzi wa jinsia moja na makahaba hupokea huduma za afya, dawa za ARV’s na kondomu.

“Tunashirikiana na makundi ya kijamii kuimarisha afya na kukabiliana na ukimwi, dawa za kulevya na unyanyapaa. Mara ya kwanza hata wahudumu wa afya walikuwa na matatizo lakini wamebadili mwenendo,” alisema.

Dkt Patta alisema endapo waraibu wa dawa za kulevya hawatotumia sindano moja kujidunga basi mamabukizi ya ukimwi itapungua.

Baadhi ya wapenzi wa jinsia moja waliohojiwa na Taifa Leo walisema wanaishi maisha ya upweke baada ya kutenwga na jamii.