Michezo

Monaco wampokeza mikoba kocha Niko Kovac

July 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Bayern Munich, Niko Kovac, amepokezwa mikoba ya kikosi cha AS Monaco kinachoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Kuteuliwa kwa Kovac kulichochewa na haja ya kujazwa kwa pengo la mkufunzi Robert Moreno Gonzalez aliyetimuliwa na Monaco mnamo Julai 19 kutokana na matokeo duni ya klabu hiyo mwanzoni mwa kampeni za msimu huu.

Kikubwa zaidi kilichochangia kufutwa kwa Kovac mnamo Novemba 2019, ni kichapo cha 5-1 ambacho Bayern walipokezwa na Eintracht Frankfurt katika Ligi Kuu ya Bundesliga mnamo Novemba 3, 2019. Kichapo hicho ndicho kilikuwa kinono zaidi kwa Bayern kuwahi kupokezwa ligini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Mchuano huo ulikuwa wa pili kwa Bayern kupoteza ligini kutokana na 10 ya ufunguzi wa msimu wa 2019-20.

Moreno ambaye ni mzawa wa Uhispania, alipokonywa mikoba ya Monaco baada ya kipindi cha miezi saba pekee.

Kovac, 48, aliwaongoza Bayern kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), taji la German Cup na ufalme wa Super Cup katika msimu wa wa 2018-19. Baada ya kufutwa kazi, nafasi yake ilitwaliwa na Hansi Flick aliyekuwa msaidizi wake.

“Kovac anafahamika sana kwa upekee wa uwezo wake wa kuongoza kikosi kusajili matokeo ya kuridhisha na kukuza wanasoka chipukizi,” akasema Naibu Rais wa Monaco, Oleg Petrov.

Moreno, 42, aliaminiwa fursa ya kudhibiti mikoba ya Monaco mnamo Disemba 2019 wakati ambapo kikosi hicho kilikuwa kikishikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1.

Monaco hatimaye waliambulia nafasi ya tisa katika Ligue 1 muhula huu wa 2019-20 baada ya msimu wa soka ya Ufaransa kufutiliwa mbali mwishoni mwa Aprili 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Kovac aliondoka uwanjani Allianz Arena wakati Bayern walipokuwa wakishikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 19, tatu nyuma ya Borussia Monchengladbach waliokuwa wakiselelea kileleni wakati huo.

Kocha huyo ambaye ni kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Croatia, alipokezwa mikoba ya Bayern mnamo Julai 2018. Katika jumla ya mechi 65 alizosimamia kambini mwa Bayern, Kovac aliwaongoza miamba hao kusajili ushindi mara 45.