Monaco yaduwaza PSG kwa kuipiga 2-0 kwenye Ligue 1

Monaco yaduwaza PSG kwa kuipiga 2-0 kwenye Ligue 1

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha AS Monaco kiliwaduwaza Paris Saint-Germain (PSG) kwa kuwapokeza kichapo cha 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumapili usiku uwanjani Parc des Princes.

Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa kocha Mauricio Pochettino kupoteza akiwa kocha wa PSG tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Thomas Tuchel aliyeyoyomea Chelsea baada ya kupigwa kalamu mnamo Disemba 24, 2020.

Sofiane Diop aliwafungulia Monaco ukurasa wa mabao katika dakika ya sita alipokamilisha krosi ya Ruben Aguilar aliyeshirikiana vilivyo na fowadi Kevin Volland.

Guillermo Maripan alizamisha kabisa matumaini ya PSG kurejea mchezoni kwa kufunga bao la pili la Monaco katika dakika ya 51 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kiungo Ander Herrera aliyeshindwa kuondoa mpira katika eneo la hatari.

Licha ya kuchezea nyumbani, PSG walielekeza kombora moja pekee langoni mwa Monaco ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 52, mbili pekee nyuma ya nambari tatu, PSG ambao ni mabingwa watetezi.

PSG walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo siku nne baada ya kuwaponda Barcelona 4-1 kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Camp Nou, Uhispania.

Nusura Monaco wanaonolewa na kocha wa zamani wa Bayern, Niko Kovac, wafunge bao la tatu katika dakika ya 60 ila Volland akazidiwa ujanja na kipa Keylor Navas.

Licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, PSG walipokezwa kichapo cha tano kufikia sasa katika kampeni za Ligue 1.

Ni pengo la alama nne kwa sasa ndilo linawatenganisha PSG na viongozi wa jedwali Lille waliowakomoa Lorient 4-1 katika mechi nyingine ya Ligue 1 mnamo Jumapili.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Februari 21):

PSG 0-2 Monaco

Montpellier 2-1 Rennes

Lens 2-1 Dijon

Nice 1-2 Metz

Nimes 2-0 Bordeaux

Strasbourg 0-0 Angers

Lorient 1-4 Lille

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Rashford awabeba Manchester United dhidi ya Newcastle...

Manchester City wazamisha chombo cha Arsenal na kuanza...