Michezo

Monaco yajitosa uwanjani kuwania huduma za Wanyama dhidi ya Club Brugge

August 24th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZIKISALIA siku 10 kabla ya kipindi kirefu cha uhamisho barani Ulaya kufungwa, tetesi zinasema kuwa klabu ya zamani ya chipukizi nyota Kylian Mbappe, AS Monaco, imejitosa uwanjani kuwania huduma za Victor Wanyama dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji.

Mabingwa mara nane wa Ufaransa, Monaco, ambao waliponea tundu la sindano kutemwa kutoka Ligi Kuu msimu 2018-2019, wameanza msimu mpya vibaya baada ya kupoteza dhidi ya Lyon na Metz kwa mabao ya kufanana 3-0.

Ingawa Club Brugge kutoka Ubelgiji inaonekana kabisa itakuwa makao mapya ya Wanyama, ambaye Spurs inataka kuuza kwa kati ya Sh1.2 bilioni na Sh1.5 bilioni baada ya kupunguza bei kutoka Sh2.1 bilioni, ripoti nchini Ufaransa zinasema kuwa Monaco tayari imewasiliana na waajiri wake Tottenham Hotspur.

“Monaco pia inamezea mate Franck Kessie wa klabu ya AC Milan na Mario Lemina kutoka Southampton, lakini imeelekeza macho yake kwa Wanyama kutafuta kiungo.

Inasemekana kuwa Monaco imeshawasiliana na Tottenham Hotspur kuhusu uwezekano wa kuajiri Wanyama,” tetesi nchini Uingereza zinasema.

Kujitosa uwanjani kwa Monaco kuwania huduma za Wanyama huenda kukavuruga mipango ya Brugge kumnyakua. Ligi ya Ufaransa ni mojawapo ya ligi kubwa barani Ulaya ikilinganishwa na ile ya Ubelgiji ambayo inapatikana nje ya 10-bora.

Pia, Monaco inao uwezo mkubwa kifedha. Inapatikana ndani ya orodha ya klabu 30 tajiri duniani za soka tofauti na Brugge ambayo haipatikani hata ndani ya klabu 100-bora.

Wanyama anasemekana alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na Brugge mnamo Agosti 22 na kuwa Brugge na Spurs zimekubaliana kuhusu mshahara wake.

Aidha, Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino alisema Ijumaa kuwa hajui kama Wanyama ataondoka klabu hii kutoka jijini London ama la, ingawa hakupinga uwezekano wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kuhama kabla ya Septemba 2.

Wanyama, ambaye majeraha yamekuwa yakimsumbua kwa misimu miwili, anasalia na miaka miwili katika kandarasi yake na Spurs inayomlipa mshahara wa Sh8.2 milioni. Inasemekana mshahara huu mkubwa ndiyo unatatiza Brugge kumchukua na kwamba Wanyama atahitajika kukubali kukatwa ili kufanikisha uhamisho huo.