Montreal anayochezea Wanyama yazidi kutesa wapinzani MLS

Montreal anayochezea Wanyama yazidi kutesa wapinzani MLS

Na GEOFFREY ANENE

CF Montreal imepunguza mwanya wa viongozi Philadelphia Union kutoka alama tano hadi mbili baada ya kuchabanga D.C. United 1-0 kwenye Ligi Kuu ya MLS ugani Saputo, Jumapili.

Kiungo Mkenya Victor Wanyama alikuwa nahodha wa timu hiyo inayotiwa makali na Mfaransa Wilfried Nancy.

Montreal iliongoza 1-0 wakati wa mapumziko baada ya beki Donovan Pines kujifunga dakika ya 41 akiondosha krosi hatari mbele ya lango lake.

Mshambulizi Joaquin Torres alipata fursa ya kuongeza bao la pili kupitia penalti, lakini ikapanguliwa na kipa David Ochoa dakika ya 80. Pines alisababisha penalti hiyo na kulishwa kadi nyekundu. Pande zote zilipoteza nafasi kadha nzuri ikiwemo beki Gabriele Corbo kuondosha mpira kwenye laini ya goli ya timu yake ya Montreal uliokuwa ukielekea nyavuni.

Ushindi huo wa tatu mfululizo unaimarisha alama za Montreal hadi 62 ikisalia na mechi moja dhidi ya Inter Miami hapo Oktoba 9 kukamilisha msimu wa kawaida.

Viongozi Philadelphia Union wana alama 64 baada ya kulimwa 4-0 na Charlotte kupitia mabao ya mvamizi Daniel Rios. Bao lake la tatu lilipatikana kupitia penalti iliyosababishwa na Mjerumani Kai Wagner aliyelishwa kadi nyekundu. Philadelphia, ambayo kwa mara ya kwanza ilijumuisha kiungo Mkenya Richard Odada kwenye benchi tangu imnunue kutoka Red Star Belgrade, Serbia mwezi Agosti, itamaliza msimu wa kawaida dhidi ya nambari 13 Toronto kwenye ligi hiyo ya klabu 14 ya ukanda wa Mashariki.

D.C. United ya kocha Wayne Rooney inavuta mkia kwa pointi 27.

Timu saba za kwanza kutoka ukanda wa Mashariki na idadi sawa kutoka ligi ya Magharibi zitaingia awamu ya muondoano kuamua bingwa wa MLS.

  • Tags

You can share this post!

London Marathon: Yehaulaw avunja utawala wa Kenya wa miaka...

Ruto alivyokwepa ulaghai wa kisiasa

T L