Michezo

Montreal Impact ya Wanyama yalipiza kisasi dhidi ya Toronto

September 3rd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Victor Wanyama alisaidia timu yake ya Montreal Impact kuzoa alama tatu muhimu katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Toronto kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) usiku wa kuamkia Alhamisi.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya alishuhudia Impact ya kocha Thierry Henry ikichukua uongozi kupitia kwa Rudy Camacho daika ya 14 na kulinda bao hilo hadi kipenga cha mwisho.

Beki Mfaransa Camacho alikamilisha pasi ndefu iliyopita juu ya Wanyama kutoka pembeni kushoto ndani ya kisanduku kupitia kichwa chake.

Toronto, ambayo ilikuwa imelemea wenyeji Impact 1-0 Agosti 29, ilikuwa na umilikaji mkubwa wa mpira (62) katika vipindi vyote viwili. Pia, ilitawala makombora 20-10, kiki zilizolenga langoni 6-3, kona 9-7 na krosi 34-12.

Hata hivyo, itajilaumu yenyewe kwa kuambulia pakavu. Ilipoteza penalti dakika ya 45 baada ya Alejandro Pozuelo kupasia mpira Pablo Piatti ambaye alialifunga, lakini akapatikana aliingia kisandukuni mapema kwa hivyo refa Drew Fischer akaifutilia mbali. Kipa kutoka Senegal Clement Diop alitawazwa mchezaji bora wa mechi hiyo baada ya kupangua shuti sita hatari kutoka kwa timu ya Toronto.

Baada ya mechi hiyo iliyosakatwa bila mashabiki uwanjani kutoka na janga la virusi vya corona, Impact inashikilia nafasi ya tano kwenye ukanda wa mashariki kwa alama 13 kutokana na mechi nane.

Toronto iko katika nafasi ya pili kwa alama 18, mbili nyuma ya viongozi Columbus Crew. Orlando City na Philadelphia Union zinakamata nafasi za tatu na nne mtawalia kwa alama 15. Timu nne za kwanza zimesakata mechi tisa kila kila moja kwenye ukanda huo wa timu 14.