Michezo

Montreal Impact yapata pigo katika juhudi zake MLS

October 25th, 2020 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Montreal Impact imepata pigo katika juhudi za kufuzu kushiriki awamu ya muondoano baada ya kupoteza 3-1 dhidi ya New York City mnamo Jumamosi katika msimu wa kawaida wa Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS).

Impact ya kocha Thierry Henry, ambayo imeajiri kiungo Mkenya Victor Wanyama, ilizamishwa na mabao kutoka kwa viungo Jesus Medina (dakika ya 68), Maximiliano Moralez (83) na Tony Rocha (86). Mshambuliaji Romell Quioto alifungia Impact bao la kufutia machozi dakika ya 89 uwanjani Yankee mjini New York.

Vijana wa Henry wako katika nafasi ya tisa kwenye ligi ya MLS ya kanda ya Mashariki kwa alama 23. Zikisalia michuano mitatu msimu wa kawaida wa ligi hiyo utamatike, Impact lazima ivune ushindi dhidi ya Nashville SC (Oktoba 28), Orlando City (Novemba 2) na DC United (Novemba 9) ili isibanduliwe kabla ya awamu hiyo muhimu. Timu 10 za kwanza kutoka kanda hii ya klabu 14 zitatinga awamu ya muondoano. Timu nane kutoka kanda ya Magharibi pia zitafuzu katika awamu ijayo itakayoanza Novemba 20 na kukamilika Desemba 12. Seattle Sounders anayochezea Mkenya Handawalla Bwana inashikilia nafasi ya pili kwenye kanda ya Magharibi baada ya kuzoa alama 32 kutokana na mechi 18.

Algeria

JS Kabylie anayochezea mshambuliaji Mkenya Masud Juma nchini Algeria ililemewa 2-1 dhidi ya Paradou AC katika mechi ya kirafiki Oktoba 24. Ligi Kuu ya Algeria (Ligue 1) bado haijaanza zaidi ya miezi sita tangu isitishwe kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona. Juma aliwahi kuripoti kupatikana na virusi hivyo na kupona. Alishiriki mechi ya kirafiki kati ya timu ya Harambee Stars na Chipolopolo ya Zambia ambayo wenyeji Kenya walishinda 2-1 Oktoba 9.

Belarus

Timu ya Isloch Minskly Rayon inayoajiri Mkenya Mohammed Katana Nyanje almaarufu Messi Agege, itamenyana na Rukh Brest katika Ligi Kuu ya Belarus hapo Oktoba 26. Isloch inashikilia nafasi ya saba kwenye ligi hiyo ya timu 16 kwa alama 43, pointi nne mbele ya nambari nane Rukh Brest.

Uingereza

Barnsley anayochezea beki Clarke Oduor ilitoka 1-1 dhidi ya Millwall kwenye Ligi ya Daraja ya Pili ya Uingereza hapo Oktoba 24. Oduor, 21, alicheza dakika 90 timu hiyo yake ikimaliza mechi hiyo ya saba mfululizo bila ushindi. Barnsley, ambayo iliponea chupuchupu kuteremshwa hadi Ligi ya Daraja ya Tatu msimu uliopita ilipoduwaza miamba Brentford 2-1 katika mechi ya kufunga msimu ambayo Oduor alifunga bao la ushindi, inashikilia nafasi ya 21 katika ligi hiyo ya 24 kwa alama nne.

Ireland

Cork City ilipoteza penalti ikalemewa ugenini 2-1 dhidi ya Sligo Rovers kwenye Ligi Kuu ya Jamhuri ya Ireland hapo Oktoba 24. Kiungo Muingereza-Mkenya Henry Ochieng’ alicheza mechi yake ya tatu mfululizo nzima. Cork inavuta mkia katika ligi hiyo ya timu 12 kwa alama 10 baada ya kusakata mechi 17.

Afrika Kusini

Kaizer Chiefs ilianza Ligi Kuu ya Afrika Kusini ya msimu 2020-2021 kwa kuchapwa 3-0 dhidi ya mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns hapo Oktoba 24. Chiefs imeajiri kiungo Mkenya Anthony Akumu Agay. Inavuta mkia baada ya kichapo hicho kikali kwenye ligi hiyo ya timu 16.

Uswidi

Elfsborg itajibwaga uwanjani dhidi ya wenyeji Varbergs kwenye Ligi Kuu ya Uswidi hapo Oktoba 26. Timu hiyo anayochezea beki Mkenya Joseph Okumu inashikilia nafasi ya tano kwa alama 39 kutokana na mechi 24 kwenye ligi hiyo ya klabu 16. AIK Stockholm anayochezea beki mwingine Mkenya Eric ‘Marcelo’ Ouma pia itaingia uwanjani mnamo Oktoba 26 kuzichapa dhidi ya Norrkoping. Timu ya AIK na Norrkoping zinashikilia nafasi za 10 na tatu, mtawalia.

Jonkopings Sodra, ambayo imeajiri kiungo mshambuliaji Eric Johanna Omondi inashikilia nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uswidi. Sodra imezoa alama 45 kutokana na michuano 24 kwenye ligi hiyo ya timu 16. Itapepetana na nambari saba Brage hapo Oktoba 26. Inahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kurejea kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Tanzania

Kipa Mkenya Farouk Shikalo alikuwa kitini timu yake ya Young Africans (Yanga) ikilipua Kinondoni MC 2-1 ugenini. Biashara Mara United inayonolewa na Mkenya Francis Baraza ilizamisha wenyeji Polisi Tanzania 1-0 nayo Simba SC wanaoyochezea beki Joash Onyango na kiungo Francis Kahata ilinyamazishwa 1-0 na Tanzania Prisons hapo Oktoba 23. Simba itarejea uwanjani kulimana na Ruvu Shooting mnamo Oktoba 26. Azam inaongoza ligi hiyo ya timu 18 kwa alama 21 kutokana na mechi saba ikifuatiwa na Yanga (19), Biashara Mara United (16) na mabingwa watetezi Simba (13). Mara imesakata mechi nane nayo Simba imejibwaga uwanjani mara sita.

Zambia

Kiungo Mkenya Duke Abuya alikuwa katika kikosi cha Nkana FC kilichocharaza Indeni 2-0 kupitia mabao ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Idris Mbombo na kutawazwa washindi wa kombe la Ngao ya Jamii nchini Zambia hapo Oktoba 24.