Michezo

Montreal Impact yapoteza mchezo dhidi ya Philadelphia Union

October 24th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MONTREAL Impact, Jumatatu ilipoteza mchezo 2-1 ikicheza dhidi ya wenyeji Philadelphia Union kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS).

Impact, ambayo ilichezesha Mkenya Victor Wanyama mechi nzima kwa mara ya 17 mfululizo katika mashindano yote tangu awasili kutoka Tottenham Hotspur mnamo Machi 3, ilizamishwa na magoli kutoka kwa kiungo wa Cape Verde Jamiro Gregory Monteiro Alvangera na mshambuliaji raia wa Brazil Sergio Santos yaliyopatikana dakika ya 39 na 48, mtawalia.

Timu hizi zilikuwa zimetoshana nguvu katika idara nyingi tu. Impact, ambayo inanolewa na kocha Mfaransa Thierry Henry, itajilaumu yenyewe kuangukia pua kwa sababu pia ilipata nafasi ya wazi kusawazisha dakika ya 85, lakini mvamizi wa Honduras Romell Quioto akapiga mpira nje licha ya kuchenga kipa kwa kuuinua vyema.

Quioto alikuwa amechangia pasi iliyozalishia Impact bao la kufutia machozi kutoka kwa Mwamerika Amar Sejdic dakika ya 65.

Wanyama, 29, ambaye ni mmoja wa wachezaji ghali (Sh833.5 milioni) katika ligi hiyo ya klabu 26 zilizogawanywa katika makundi ya Mashariki (14) na Magharibi (12), alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 59.

Kadi hiyo ni yake ya tatu baada ya kuonyeshwa kadi ya njano dhidi ya Toronto FC mnamo Agosti 29 na Septemba 2. Sheria za MLS zinasema kuwa mchezaji akipata kadi tano za njano katika msimu wa kawaida atapigwa faini ya Sh27,145 (Dola 250) na marufuku ya mechi itakayofuata ya ligi.

Dhidi ya Philadelphia, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya alisukuma kombora moja kali baada ya kupokonya mchezaji wa timu hiyo mpira nje ya kisanduku, lakini likakosa lango pembemba.

Impact iko katika nafasi ya nane kwa alama 20 baada ya kusakata mechi 17 katika kundi la Mashariki linaloongozwa na Toronto kwa alama 37. Philadelphia ni ya pili alama tatu nyuma.

Kundi A linaongozwa na Seattle Sounders, ambayo ilizabwa 3-1 na Los Angeles FC ugenini. Sounders imeajiri Mkenya Handwalla Bwana ambaye alikosa mechi hiyo.

Ligi hiyo iliahirisha mechi tatu wikendi iliyopita ya Oktoba 10-11 baada ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa kambini mwao. Mechi hizo zilikuwa kati ya Orlando City na Columbus Crew, FC Dallas na Minnesota United, na  Colorado Rapids na LA Galaxy.