Michezo

Montreal Impact yazoa ushindi wa kwanza katika mechi 6, Seattle yasalia juu

October 8th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Montreal Impact inayoajiri Victor Wanyama na Seattle Sounders anayochezea Handawalla Bwana zimevuna ushindi muhimu kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) dhidi ya Columbus Crew na Real Salt Lake usiku wa kuamkia Alhamisi, mtawalia.

Impact ya kocha Thierry Henry, ambayo ilinunua nahodha wa timu ya taifa ya Kenya Wanyama kutoka Tottenham Hotspur nchini Uingereza mapema Machi 2020, ilizamisha Columbus 2-1 kupitia mabao ya wachezaji Lassi Lappalainen na Bojan Krkic.

Lappalainen aliweka Impact kifua mbele dakika ya 24 kabla ya Krkic kufunga bao la ushindi kupitia penalti dakika ya 74 baada ya Mhispania huyo kuangushwa ndani ya kisanduku. Gyasi Zardes alikuwa amesawazisha dakika ya 45.

Wenyeji Columbus walitawala idara zote za mchezo huo ikiwemo makombora yote 19-8, makombora yaliyolenga lango 5-3, umilikaji wa mpira 59-41, pasi 452-333 na kona 3-0. Hata hivyo, Impact iliongoza katika kusababisha ikabu 17-6 ishara kuwa ilijitahidi vilivyo katika kuzima mashambulizi.

Impact iliingia mchuano huo ikiwa katika nafasi ya tisa alama 14 nyuma ya viongozi wa ligi ya MLS ya ukanda wa Mashariki Columbus, ambao pia walikuwa wamelemea vijana wa Henry 2-1 mnamo Julai 21. Columbus pia haikuwa imepoteza nyumbani dhidi ya Impact katika mechi sita zilizopita kabla ya kupigwa breki Oktoba 8. Ushindi wa Impact imeiwezesha kupaa nafasi mbili hadi nafasi ya nane. Imezoa alama 20 kutokana na ushindi sita, sare mbili na vichapo vinane.

Columbus imepoteza uongozi na sasa inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 31 baada ya kusakata mechi 16. Toronto FC na Philadelphia Union zinashikilia nafasi mbili za kwanza kwa alama 34 na 31, mtawalia. Toronto ililemea nambari sita New England Revolution 1-0 nayo Philadelphia ikalima FC Cincinnati 3-0. Seattle Sounders imefungua mwanya wa alama tatu juu ya ligi ya MLS ya ukanda wa Magharibi baada ya kuchapa Real Salt Lake na kufikisha alama 30 baada ya mechi 15. Wanyama alichezea Impact mechi nzima naye Handawalla alikuwa kitini.

Impact itarejea uwanjani Oktoba 12 kumenyana na wenyeji Philadelphia nayo Seattle Sounders pia itakuwa ugenini siku hiyo dhidi ya nambari tano Los Angeles FC.