Montreal yanufaika na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Noble Okelo kuliza Toronto ligini

Montreal yanufaika na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Noble Okelo kuliza Toronto ligini

Na GEOFFREY ANENE

CF Montreal anayochezea Mkenya Victor Wanyama imedumisha rekodi ya kutoshindwa hadi mechi nne kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) baada ya kulipua mahasimu wa tangu jadi Toronto 3-1 ugani Saputo mnamo Agosti 28.

Wenyeji Montreal walipata nguvu zaidi ya kuhangaisha wenzao hao kutoka Canada baada ya kiungo Noble Okelo mwenye asili ya Uganda kulishwa kadi nyekundu alipomkanyaga Wanyama dakika ya tano.

Hata hivyo, licha ya Toronto kusalia watu 10, Montreal ilihitaji kuweka presha kabisa hadi dakika ya 23 kufungua ukurasa wa magoli kupitia kwa kiungo Samuel Piette.

Kipa Quentin Westberg alikuwa amepangua frikiki ya Djordje Mihailovic, lakini ikaelekea alikokuwa nahodha Piette ambaye hakukosea kutikisa nyavu.

Hakuna magoli zaidi yalishuhudiwa tena katika kipindi cha kwanza kabla ya Toronto kusawazisha 1-1 kupitia kwa Ifunanyachi Achara dakika ya 58 baada ya kupokea pasi safi ndani ya kisanduku kutoka kwa Yeferson Soteldo.

Joaquin Torres, ambaye alikuwa amepoteza nafasi nzuri katika kipindi cha kwanza, alifungia Montreal bao la pili dakika 10 baadaye alipopokea pasi murwa kutoka kwa Zachary Brault-Guillard. Beki Brault-Guillard alipumzishwa dakika ya 73, huku kocha Wilfried Nancy akijaza nafasi yake kwa kuingiza Zohran Bassong.

Dakika mbili baadaye, Montreal, ambayo ilichapa Toronto 4-2 zilipokutana mapema msimu huu wa 2021 mwezi Aprili, ilikamilisha maangamizi kupitia kwa Romell Quioto dakika ya 75. Mshambuliaji huyo wa Honduras alikuwa akirejea kutanda soka baada ya kukosa michuano tisa akiuguza jeraha.

Montreal inashikilia nafasi ya sita kwa alama 31 baada ya kujibwaga uwanjani mara 22 kwenye ligi ya MLS ya ukanda wa Mashariki. Toronto inavuta mkia (nambari 14) kwa alama 15 baada ya kusakata mechi 22. Imepoteza mechi nne mfululizo. Timu saba za kwanza kutoka ukanda huo na idadi sawa kutoka ukanda wa Magharibi zitaingia awamu ya muondoano.

You can share this post!

PSG kuweka mezani Sh13 bilioni kwa ajili ya Richarlson...

Lady Doves ya Uganda yaanza Cecafa kwa kulipua FAD ya...