Michezo

Moraa atawala Doha Diamond League

May 11th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia na Jumuiya ya Madola mbio za mita 800, Mary Moraa ametwaa taji la riadha za Diamond League duru ya Doha nchini Qatar.

Moraa, ambaye ni bingwa wa Kenya mbio za 400m na 800m, alinyakua taji la Doha katika ziara yake ya kwanza baada ya kukamilisha mizunguko hiyo miwili kwa dakika moja na sekunde 57.96.

Kwenye orodha ya watimkaji 11, afisa huyo wa polisi amefuatiwa kwa karibu na Muingereza Jemma Reekie (1:58.42) na raia wa Benin Noelie Yarigo (1:58.70) waliozoa nishani ya fedha na shaba kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini mwezi Machi, pamoja na Muethiopia Habitam Alemu (1:59.08) na bingwa wa dunia mwaka 2019 Halimah Nakaayi kutoka Uganda (1:59.48), mtawalia.

Moraa, ambaye mwezi Aprili alitawala Kip Keino Classic jijini Nairobi, anapanga kuvizia rekodi ya dunia ya 600m wakati wa mashindano ya USAF Los Angeles Grand Prix mnamo Mei 9 nchini Amerika kabla ya kutimka mbio za 800m kwenye Eugune Diamond League mnamo Mei 25 nchini humo.

Washiriki wengine kutoka Kenya jijini Doha ni bingwa wa dunia wa kurusha mkuki mwaka 2015 Julius Yego, mfalme wa mbio za 1500m mwaka 2019 Timothy Cheruiyot na bingwa wa dunia na Afrika wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 wa umbali huo Reynold Cheruiyot pamoja na Abel Kipsang na Brian Komen.

Pia, kuna bingwa wa mbio za nyika duniani na Jumuiya ya Madola mbio za 5000m Beatrice Chebet pamoja na Grace Loibach na Christine Njoki.

Bingwa wa zamani wa Michezo ya Afrika Benjamin Kigen atapimana ubabe na Amos Serem, Abraham Kibiwot na Wilberforce Kones katika mbio za 3000m kuruka viunzi na maji ambapo wana kibarua dhidi ya Waethiopia.

Bingwa wa Diamond League inayojumuisha duru 15 (Xiamen, Shanghai/Suzhou, Doha, Rabat/Marrakech, Eugene, Oslo, Stockholm, Paris, Monaco, London, Lausanne, Silesia, Rome, Zurich na Brussels), atatia mfukoni Sh3.9m.

Mshindi wa kila duru anatia kibindoni Sh1.3 milioni.