Michezo

Morans jogoo wa Tusker Safari baada ya kuilaza Afrika Kusini

October 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MORANS ilihakikisha taji la raga ya wachezaji saba kila upande ya kimataifa ya Tusker Safari Sevens linarejea Kenya baada ya kuduwaza miamba Afrika Kusini kwa alama 19-14 Jumapili katika fainali ya kusisimua uwanjani RFUEA jijini Nairobi.

Timu hii ya pili ya Kenya ililipiza kisasi kwa kichapo cha alama 19-5 ambacho timu ya kwanza ya Kenya almaarufu Shujaa ilipokea dhidi ya Afrika Kusini katika nusu-fainali.

Morans, ambayo pia ilikutana na Afrika Kusini katika mechi za makundi na kulazwa 17-12 Jumamosi, ilijiweka pazuri kutwaa taji ilipoongoza 19-0 wakati wa mapumziko kupitia miguso ya Geoffrey Okwach (miwili) na Alvin Otieno (mmoja) na mkwaju wa Johnstone Olindi.

Afrika Kusini ilifuta machozi na miguso miwili na mikwaju dakika ya mwisho.

Shujaa iliridhika na nafasi ya tatu baada ya kulima Russia Academy ya nyota wa Fiji, Waisale Serevi.

Katika nusu-fainali, Afrika Kusini iliongoza KCB 26-0 wakati wa mapumziko ikiibuka na ushindi wa 31-14 katika robo-fainali. Shujaa ilitolewa kijasho chembamba na mabingwa watetezi Samurai kabla ya kuwalemea 19-14 katika mechi ambayo nyota Collins Injera aliumia.

Matokeo (Oktoba 20):

Fainali – Afrika Kusini 14-19 Morans;

Nambari tatu – Shujaa 19-5 Russia Academy;

Nusu-fainali kuu – Afrika Kusini 19-5 Shujaa, Morans 24-10 Russia Academy;

Fainali ya nambari tano – Seventise 19-10 Samurai;

Nusu-fainali ya nambari tano hadi nane – KCB 17-21 Samurai, Seventise 21-7 Red Wailers;

Robo-fainali kuu – Afrika Kusini 31-14 KCB, Shujaa 19-14 Samurai, Morans 24-7 Seventise, Red Wailers 5-17 Russia Academy;

Challenge Trophy (fainali) – Western Province 29-12 Uganda;

Challenge Trophy (nusu-fainali) – Uganda 26-21 Zambia, Uhispania 5-22 Western Province;

Challenge Trophy (robo-fainali) – Uganda 17-12 Zimbabwe, Zambia 27-17 Zastava, Uhispania 48-5 Burundi, Western Province 33-26 Blue Bulls; Fainali ya nambari 13 – Narvskaya Zastava 21-38 Blues Bulls;

Nusu-fainali ya nambari 13 hadi 16 – Zimbabwe 10-14 Narvskaya Zastava, Burundi 0-64 Blue Bulls.