Michezo

Morans kutegemea wanavikapu wa majuu

July 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI Cliff Owuor wa Kenya Morans anafukuzia huduma za wanavikapu wawili mahiri wanaochezea nchini Amerika kadri anavyolenga kukisuka kikosi chake kwa minajili ya mapambano ya Novemba ya kufuzu kwa fainali za bara Afrika za FIBA Afro-Basket mnamo 2021.

Wachezaji hao kwenye rada kali ya Owuor ni Alonzo Ododa na Preston Bungei. Ododa ni mwanawe mwanavikapu wa zamani wa kimataifa Sebastien Ododa ambaye hadi kuondoka kwake humu nchini na kuyoyomea Amerika, aliwahi kuvalia jezi za Posta na KCB Lions.

“Ninawafuatilia wachezaji hawa wawili kupitia wakufunzi wao nchini Amerika. Itakuwa afueni kubwa kwa Morans iwapo tutafaulu kuwashawishi kuwa sehemu ya kampeni zijazo za Afro-Basket jijini Kigali, Rwanda,” akasema Owuor anayepania kusuka kikosi chenye mseto wa wanavikapu wa humu nchini na wa kimataifa.

Zaidi ya Ododa na Bungei, kocha Owuor amefichua kuwa anamhemea mwanavikapu Desmond Owili anayechezea nchini Australia.

Morans watafungua kampeni zao za Kundi B za kuwania taji la FIBA Afro-Basket dhidi ya Senegal mnamo Novemba 27. Kenya wamepangiwa kupepetana na Angola mnamo Novemba 28 katika mchuano wao wa pili kabla ya kufunga mechi za makundi kwa kupimana ubabe na Msumbiji mnamo Novemba 29.

Mkondo wa pili ya kipute cha Afro-Basket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, wanavikapu wa Owour watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.

Jumla ya vikosi 20 vitapangwa katika makundi matano ya vikosi vinne kwa minajili ya mechi za raundi ya pili ya mchujo. Washindi watatu wa kwanza kutoka kila kundi watajikatia tiketi za kushiriki fainali za FIBA Afro-Basket nchini Rwanda.

Chini ya Owuor, Kenya inalenga kunogesha fainali za kipute hicho cha haiba kubwa barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1993.

“Napania kuwaita kambini wanavikapu wangu wote pamoja na wale walioko ughaibuni kwa maandalizi ya mapema yatakayoweka hai matumaini yetu ya kujitwalia ubingwa wa Afro-Basket. Ilivyo, sioni kizingiti kikubwa katika safari ya kufikia mafanikio hayo,” akasema Owuor.

Kati ya mikakati yake ya kujifua kwa kivumbi hicho, Owuor amefichua kwamba vijana wake wamepangiwa mechi za kirafiki dhidi ya Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Michuano hiyo itaanza pindi janga la corona litakapodhibitiwa vilivyo na mataifa hayo husika kulegeza kanuni za usafari wa kimataifa.

Mnamo 1993, Morans waliambulia nafasi ya nne kwenye vikapu vya Afro-Basket licha ya kuwa wenyeji wa kipute hicho jijini Nairobi. Mnamo 2019, kikosi hicho kiliduwaza miamba wa bara la Afrika kwa kutinga fainali za kivumbi hicho nchini Mali japo wakazidiwa maarifa na DR Congo.

Chini ya nahodha Griffin Ligare, Morans walifuzu kwa fainali baada ya kutawala kundi la washindani sita kwenye mchujo ulioandaliwa uwanjani Nyayo, Nairobi. Wakichuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani, Morans waliwabwaga Burundi, Eritrea, Sudan Kusini, Somalia na Tanzania.