Michezo

Morans walakiwa kishujaa baada ya kutia fora vikapuni

July 30th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Kenya almaarufu Morans ililakiwa kwa shangwe na nderemo Jumatatu kutoka nchini Mali ilikozoa medali ya fedha kwenye mashindano ya Bara Afrika ya AfroCan.

Wachezaji densi wa Isukuti na wale kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi walitumbuiza vijana hao wa kocha Cliff Owuor pamoja halaiki ya watu iliyojitokeza kusherehekea matokeo hayo ya kihistoria.

Katibu katika Wizara ya Michezo Kirimi Kaberia, Kamishna wa Michezo Japson Gitonga na Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Vikapu la Kenya (KBF) Paul Otula pamoja na mashujaa hao wapya wa Kenya walikuwa miongoni mwa watu walioshindwa kujizuia kucheza densi kutokana na nyimbo tamu zilizoporomoshwa.

Maombi yalifuatia densi hiyo na kisha hotuba za kusifu Morans kutoka kwa Otula na Kaberia kabla ya mabingwa hawa wa Ukanda wa Tano kuabiri malori matatu makubwa kutoka kundi la Sonko Rescue Team yaliyokodishwa kuwapa mapokezi hayo ya kishujaa hadi katikati mwa jiji chini ya ulinzi wa polisi.

Msongamano wa magari kwenye Barabara Kuu ya Mombasa ambao kwa kawaida huwa mkubwa, uliongezeka kutokana na msafara wa magari zaidi ya kumi yaliyozungusha Morans jijini Nairobi, huku Wakenya wakisherehekea ufanisi huo ambao haukuwa umewahi kushuhudiwa na Kenya.

Otula alimiminia sifa tele serikali pamoja na wadhamini wakiwemo Badoer Investment ambao wanafadhili KBF kwa Sh20 milioni kila mwaka kwa miaka mitano na pia walivalisha Morans jezi za timu ya taifa.

Alisema Mungu alikuwa na Morans katika safari yake yote na kuongeza kuwa, “Isingekuwa Mungu, Wakenya hawangekuwa wakisherehekea ufanisi huo.”

Alikiri kuwa Morans ilifanya vizuri kutokana na kudumisha nidhamu aliyotaja kuwa ya aina yake.

“Nidhamu iliwafikisha pale wamefika leo hii. Akili zao zote zilikuwa katika kuwakilisha Kenya,” alisema Otula.

Kwa upande wake, Kaberia alisema kuwa serikali itasimama na Morans na kuendelea kuipatia usaidizi.

Alifurahishwa kuona fani tofauti zikiinuka kutoka Kenya mbali na riadha zikiwemo mpira wa vikapu, mbio za magari za Safari Rally, timu ya raga ya chipukizi almaarufu Chipu na hata Harambee Stars iliyoshiriki Kombe la Afrika (AFCON) wiki chache zilizopita nchini Misri.

“Timu ya Morans inaonyesha kuwa Kenya inapiga hatua nzuri mbele kimchezo,” alisema afisa huyo na kukiri kuwa serikali ya kitaifa haiwezi kazi ya kuimarisha michezo pekee yake.

Sifa kwa Sonko

Alimsifu Gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa kuwa katika mstari wa mbele katika kuunga mkono michezo na kutoa changamoto kwa magavana wengine pamoja na kampuni za kibinafsi kufuata mkondo huo.

“Bila ya usaidizi wao, serikali haitafaulu kutimiza mahitaji yote ya timu zetu za taifa. Tungependa kukumbusha wadhamini kuwa wakisaidia timu zetu watanufaika na ushuru wa chini,” alisema Kaberia.

Otula alirai kampuni za kibinafsi kushirikiana na serikali kukuza talanta akisema kuwa Kenya imebarikiwa na talanta tele jinsi Morans imethibitisha.

Mfungaji bora wa makala hayo ya kwanza ya AfroCan, Tylor Okari alifichua kuwa wamejifunza mengi kutoka kwa mashindano hayo na watafanya vyema zaidi wakipatana na DR Congo tena ambayo ndiyo timu pekee ilitwaa ushindi dhidi ya Kenya nchini Mali.

Morans iliandiliwa kiamsha kinywa na dhifa ya chakula cha mchana na wadhamini na pia kutunukiwa Sh1 milioni na Gavana Sonko.