Michezo

Morans wang’atwa na ‘The Lions’ ya Senegal mechi za kuingia AfroBasket zikianza Rwanda

November 25th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Morans imeanza vibaya kampeni ya kurejea katika Kombe la Afrika la mpira wa vikapu la wanaume (AfroBasket) baada ya kuwa nje miaka 23 kwa kupepetwa kwa alama 92-54 jijini Kigali nchini Rwanda mnamo Novemba 25.

Washindi wa medali ya fedha ya Afrika kwa mashindano ya wachezaji wanaocheza mpira wa vikapu barani humu (AfroCan) Morans waliwapa Wakenya matumaini wanaweza kusumbua ‘simba’ wa Senegal katika robo ya kwanza ambayo ilikuwa nipe-nikupe na kutamatika 19-19.

Hata hivyo, vijana wa kocha Cliff Owuor walipoteza mwelekeo katika robo ya pili waliyopoteza 28-14.

Morans walijaribu kurejea mechini katika robo ya tatu waliyoshinda 19-11, lakini wakashindwa kabisa kuziba mwanya wa kati ya sita na 10 katika robo hiyo kabla ya kuzidiwa maarifa kabisa katika robo ya mwisho 34-2.

Pasi kadha mbovu, kupeana ikabu ovyovyo pamoja na kupoteza nafasi za kadhaa nzuri za kufunga kulichangia pakubwa katika Morans kupokea kichapo hicho cha tatu mfululizo mikononi mwa Senegal katika historia ya mashindano haya.

Isitoshe, wapinzani wao, ambao walibwaga Morans 91-58 katika mechi za makundi na 90-76 katika mechi ya kuamua mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya AfroBasket jijini Nairobi mwaka 1993, walikuwa wazuri sana katika kufunga alama tatu, kupata ikabu na kulinda ngome yao.

Clevin Hannah alikuwa ‘muuaji’ wa timu ya Kenya alipochangia pointi 12, pasi tisa zilizozalisha alama pamoja na kuiba mpira mara moja.

Mfungaji bora katika mchuano huo wa kufungua mashindano hayo ya Kundi B kwa upande wa Kenya alikuwa Mkenya Tylor Okari anayechezea Bakken Bears nchini Denmark. Okari alipachika alama 13, kumega pasi tano zilizofungwa na kuiba mpira mara mbili. Ibrahima Faye alipachika alama nyingi kwa upande wa Senegal na pia mechi hiyo (19).

Kenya ilizidiwa ujanja katika ufungaji wa alama mbili (two-pointer) kwa asilimia 59 dhidi ya 31, alama tatu (three-pointer) kwa asilimia 47-21 na pia alama za ikabu kwa asilimia 66-50.

Kabla ya mechi hii, Kenya ilipata pigo wakati Mwamerika-Mkenya Preston Bungei, ambaye anacheza mpira wa vikapu nchini Australia, alipofungiwa nje ya mashindano na Shirikisho la Mpira wa Vikapu barani Afrika (FIBA Africa) kwa sababu alikosa pasipoti ya Kenya. Ni mmoja wa wachezaji ambao Owuor alitumai kutegemea katika mashindano haya.

Bush Wamukota, ambaye alicheza mpira wa vikapu wa malipo nchini Rwanda, naye yuko karantini nchini DR Congo alikokuwa ameenda kushiriki mashindano. Mchezaji bora wa Kenya katika mechi za kuingia awamu hii ya mwisho ya kufuzu kushiriki AfroBasket, Griffin Ligare naye hatimaye alipata ruhusa kutoka kwa waajiri wake, ingawa anafaa kuwa karantini saa 24 baada ya kuwasili nchini Rwanda mnamo Jumatano adhuhuri.

Ligare huenda akatumiwa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Angola katika mechi ya pili ya Kenya hapo Novemba 26. Mechi hiyo pia inatarajiwa kuwa ngumu kwa Morans, ambayo ilicharazwa 110-40 ilipokutana na Angola katika mechi za makundi za AfroBasket mwaka 1989 jijini Luanda.

Mechi ya mwisho ya Kenya itakuwa dhidi ya Msumbiji hapo Novemba 27. Timu hizi nne zitarudiana Februari 2021, huku tatu za kwanza zikijikatia tiketi ya kushiriki AfroBasket baadaye mwaka 2021 jijini Kigali.