Michezo

Morata abeba Juventus hadi hatua ya 16-bora katika UEFA

November 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BAO la dakika ya mwisho wa kipindi cha pili kutoka kwa mshambuliaji Alvaro Morata lilisaidia Juventus kuzamisha chombo cha Ferencvaros ya Hungary kwa mabao 2-1 na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 24, 2020.

Ferencvaros ambao ni miamba wa soka ya Hungary walijiweka uongozini katika dakika ya 19 kupitia kwa Myrto Uzuni kabla ya nyota Cristiano Ronaldo kusawazisha mambo katika dakika ya 35.

Bao hilo la Ronaldo ambaye pia amewahi kuchezea Manchester United na Real Madrid lilikuwa lake la 749 kitaaluma.

Ingawa Juventus walitamalaki mchezo katika kipindi cha pili, juhudi zao zilikosa kuzaa matunda hadi dakika ya 90 ambapo Morata alimwacha hoi kipa Denes Dibusz.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi G kwa alama tisa, tatu nyuma ya viongozi Barcelona. Kyiv waliopigwa 4-0 na Barcelona wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi moja sawa na Ferencvaros wanaovuta mkia.