Michezo

Morata afunga mawili katika mechi yake ya 100 kambini mwa Juventus na kusaidia miamba hao wa Serie kulaza Ferencvaros

November 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ALVARO Morata alifunga mabao mawili na kusaidia miamba wa soka ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Juventus kuwapepeta wapambe wa soka ya Hungary, Fenecvaros 4-1 kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 4, 2020.

Nyota Cristiano Ronaldo alimwandalia pasi Morata akifunga bao lake la pili.

Juventus ya kocha Andrea Pirlo ilishuka dimbani ikiwa na hamu ya kujinyanyua baada ya kupigwa 2-0 na Barcelona kwenye mechi ya awali ya Kundi G katika UEFA jijini Turin.

Morata aliwaweka Juventus uongozini kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa yake ya 100 ndani ya jezi za kikosi hicho kunako dakika ya saba kabla ya kupachika wavuni goli la pili kunako dakika ya 60.

Mabao mengine ya Juventus yalifumwa wavuni kupitia kwa Paulo Dybalo katika dakika ya 72 kabla ya Lasha Dvali kujifunga mwishoni kwa kipindi cha pili.

Ferencvaros walifutiwa machozi na Franck Boli sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Morata kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa kivumbi cha UEFA hadi kufikia sasa msimu huu kwa pamoja na Marcus Rashford wa Manchester United na Diogo Jota wa Liverpool.

Katika mchuano mwingine wa Kundi G, Barcelona waliendeleza rekodi ya asilimia 100 kwenye kampeni za UEFA msimu huu ka kuwatandika Dynamo Kyiv kutoka Ukraine 2-1 uwanjani Camp Nou, Uhispania.