Makala

MOSES OTIENO EGESA: Mtunzi wa muziki wa injili anayelenga juu

May 22nd, 2018 2 min read

Na PATRICK KILAVUKA

KUJIPA matumaini ni kujiweka katika hali ya kutarajia. Ni katika kutumaini na kuvumilia, dau lake la kukuza kipawa chake cha uimbaji lilijibiwa.

Msanii Moses Otieno Egesa anasema ombi lake lilikuwa siku moja awe mwimbaji anayesifika na kwa kweli Maulana kamjibu kupitia kushiriki katika shindano ambalo lilimtoa mavumbini kitalanta.

Nyota yake ya jaha iling’ara katika shindano la Exdous Talents Awards wakati alipolinogesha shindano hilo la kusaka talanta la makala ya Siaya ambalo lilifanyiwa kanisa la Chrisco, Ukwala, kaunti ndogo ya Ugenya akiimba wimbo Sina Mungu Mwengine wa Reuben Kigame na Sifa Voices.

Katika kategoria ya wanaume, alikuwa kidedea na kutawazwa mwimbaji bora wa kiume wa mwaka 2018 na kutuzwa vyeti na kikombe.

Shindano hilo liliandaliwa na msanii Cosmus K na lilimwezesha kupewa fursa ya kurekodi muziki, kujitambua zaidi kisanii na kutuzwa kikombe na vyeti kama njia ya kuchochea vipaji mashinani.

Moses Egesa Exdous alipotuzwa cheti kwenye shindano la Talents Awards mjini Siaya. Picha/ Patrick Kilavuka

Msaniii Otieno, 24, ni mwanachuo wa mwaka wa pili, masuala ya Sayansi ya Siasa na Usimamizi wa Umma,  Chuo Kikuu cha Rongo, bewa la mjini,na anatoka Port Victoria, kaunti ndogo ya Budalang’i, Kaunti ya Busia.

Anasema fursa aliyopewa ya kurekodi muziki wake, inaashiria hatua ya kuendeleza ndoto yake ya kuwa msanii mahiri na anatumaini kwamba, kupitia muziki wa injili atafikia mbali.

“Sikutarajia ningerekodi haraka hivyo! Lakini mipango ya Mola, haipigiwi mfano,” asema msanii huyo ambaye amerekodi nyimbo zake mbili kupitia ufadhili wa muafaka wa muandalizi wa shindano hilo.

Fauka ya hayo, alihimizwa na wachungaji wake Bw na Bi Martin Josiah wa kanisa la Chrisco, Ugenya, Kaunti ya Siaya ambako anasomea chini ulezi wa shangazi yake kujitosa katika shindano hilo na akajisajili.

“Mchungaji alinishawishi kutupa ndoano katika shindano hilo pasi na kujua kwamba, ilikuwa neema ya kujinasia ufadhili wa kurekodi muziki wangu, ” anakiri Otieno ambaye alianza kuimba akiwa na miaka kumi katika ibada ya watoto ya shule ya Jumapili kanisa la Pentecostal, Mukoma  ambako nyanya yake Leonida Bwire alikuwa anashiriki.

Pia, Shule ya Msingi ya Mukoma kabla kujiunga na Sekondari ya Budalangi.

Ingawa ana nyimbo kumi na tano ambazo amezitunga kwa minajili ya kuzirekodi, amezinasa mbili chini ya ufadhili.

Msanii Moses Egesa alipoibuka kidedea na kutawazwa mwimbaji bora wa kiume wa mwaka 2018. Picha/ Patrick Kilavuka

Nazo ni Sina Mwengine Wakumwabudu (unaelezea ushuhuda wake na matendo ya Mungu kupitia neema yake) na Mwaminifu Akisema Atatenda- ukiwa na ujumbe wa kuwatia moyo waja kumtegemea Mola pasi na kukata tamaa maishani kwani akisema haghairi na hutimiza.

Nyimbo zingine ni Nimewasamehe, Wakuabudiwa, Open My Eyes, Majesty, Bow Down as We Worship na kadhalika.

Anasema nyimbo zake nyingi amezitunga baada ya kujiunga na chuo kikuu ambako yeye pia kiongozi wa muungano wa wakristo chuoni .

Mada ambayo huilenga katika utunzi wake ni kuelezea waja namna ilivyo bora kumwabudu Mungu Muumba pekee kama njia ya kumrudishia sifa na utukufu.

Manufaa ya uimbaji? Anadokeza kwamba  hujikimu akipata mialiko au shoo na humsaidia nyanya yake ambaye amekuwa msaada mkubwa katika malezi.

Mbali na kuwasaidia dada na ndugu zake, ametambuliwa, amepata fursa ya kunakili muziki wake, milango na matumaini ya kustawisha uwanda wa muziki kuonekana kuwa uhai

Angependa kuwashukuru mapasta ambao wamemlea  kiroho na kukuza kipaji chake Bw na Bi Josiah, wadau wa shindano la kukuza talanta na marafiki ambao humtia hamasa ya kuchochea kipawa chake.

Ushauri wake ni kwamba mtagasuano wa watu huwapelekea kuwiana kwa namna mbalimbali na kuyafikia malengo yao maishani, kitalanta na kitaaluma.