Habari Mseto

Motego, Obiri kutawazwa mashujaa na kaunti

October 19th, 2020 1 min read

BENSON AYIENDA na RUTH MBULA

MCHEZAJI wa zamani wa timu ya taifa, Harambee Stars, Henry Motego na Bingwa wa Dunia wa mbio za mita 5,000 Hellen Obiri watatambuliwa rasmi kama mashujaa na serikali ya Kaunti ya Kisii wakati wa Sherehe za Mashujaa kwenye uwanja wa michezo wa Gusii, Jumanne.

Wanariadha wengine wa zamani watakaotambuliwa ni Yobes Ondieki na marehemu Nyantika Mayioro.

Gavana wa Kisii James Ongwae alisema kuwa kaunti itawatambua wanariadha hao kutokana na mchango wao katika kutangaza Kenya katika rubaa za kimataifa.

Alisema serikali yake inalenga kuboresha sekta ya michezo nchini.

“Mchango wao katika michezo ni wa kupigiwa mfano. Mbali na kuwatambua mashujaa hao, tumekarabati uwanja wa michezo wa Gusii na utatumiwa na wanamichezo mbalimbali kukuza vipaji vyao,” akasema.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza hafla hiyo.

Motego alikuwa mchezaji wa Harambee Stars na timu ya Shabana na anakumbukwa kutokana na weledi wake katika ufungaji wa mabao.

Obiri ni miongoni mwa wanariadha waliofana zaidi humu nchini. Ondieki alitamba katika mbio za mita 5,000 katika miaka ya 1990.

Maiyoro ni miongoni mwa Wakenya wa kwanza kujitosa katika mashindano ya kimataifa katika miaka ya 1950 na 1960.

Motego, 56, alikuwa miongoni mwa wanasoka waliocheza nje ya bara la Afrika baada ya kuichezea timu ya

Al-Oruba ya nchini Oman mnamo 1992.

Mwanasoka huyo wa zamani sasa ni meneja wa wizara ya michezo wa Kaunti ya Kisii ambapo anafanya kazi ya kukuza vipaji.