Motisha tele kambini mwa Kenya Morans baada ya mwanavikapu Wamukota anayechezea Amerika kuwasili

Motisha tele kambini mwa Kenya Morans baada ya mwanavikapu Wamukota anayechezea Amerika kuwasili

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya Morans kimepigwa jeki na ujio wa kiungo matata Tom Wamukota ambaye anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanavikapu tegemeo katika kampeni za mkondo wa pili za kufuzu kwa Kombe la Afrika la Afro-Basket jijini Yaounde, Cameroon.

Mechi hizo zimeratibiwa kupigwa kati ya Februari 17-21, 2021.

Kocha msaidizi wa Morans, Sadat Gaya amethibitisha kwamba Wamukota, aliyekosa mkondo wa kwanza jijini Kigali, Rwanda mnamo Novemba 2019, sasa yuko jijini Nairobi.

“Wamukota amewasili kutoka Amerika anakochezea kikosi cha Ronnie Gundo. Anatarajiwa kuanza kushiriki mazoezi ya pamoja na kikosi mapema wiki ijayo,” akasema Gaya.

Wamukota alikosa kuwa sehemu ya kampeni za mkondo wa kwanza za Morans baada ya kuzuiliwa kuondoka nchini DR Congo na kutua Rwanda mnamo Novemba kwa sababu ya kanuni kali za kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

“Analeta tajriba pevu na uzoefu mpana kambini mwa Morans. Ana sifa za kukiongoza kikosi na uwepo wake utazidisha viwango vya ushindani kambini mwetu,” akasema Gaya kuhusu kiungo huyo anayejivunia urefu wa futi saba.

Mnamo Januari, Wamukota alikuwa tegemeo la Morans katika mechi za kufuzu kwa raundi ya sasa ya Afro-Basket. Nyota huyo aliyetamba zaidi dhidi ya Sudan Kusini, alikuwa akichezea kikosi cha Patriots nchini Rwanda wakati huo.

Ni matarajio ya Gaya kwamba ushirikiano kati ya Wamukota na Desmond Owili ambaye sasa amepona jeraha alilolipata jijini Kigali, utatambisha sana kikosi cha Morans nchini Cameroon. Owili kwa sasa hucheza vikapu vya kulipwa nchini Australia na anatarajiwa pia kuwasili nchini na kuingia kambi ya mazoezi wiki ijayo.

Kenya inalenga kufuzu kwa fainali za Afro-Basket kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27. Morans watafungua kampeni zao za mkondo wa pili katika Kundi B mnamo Februari 19 kwa kuvaana na Senegal ambao ni viongozi wa kundi hilo.

Wameratibiwa kupepetana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia na Msumbiji katika siku ya mwisho. Mechi nyinginezo za kufuzu zimepangiwa kuandaliwa jijini Monatsir, Tunisia ambapo jumla ya vikosi 16 vitanogesha fainali za Fiba Afro-Basket jijini Kigali mnamo Agosti, 2021.

You can share this post!

Raila ataka serikali ilegeze masharti ya ibada

Madiwani zaidi ya 50 Murang’a waelezea kuunga BBI