Habari za Kitaifa

Moto shuleni Kirogo waacha wanafunzi 200 bila mabweni

February 3rd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

ZAIDI ya wanafunzi 200 wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kirogo katika Kaunti ya Murang’a wameachwa bila malazi baada ya moto kuteketeza mabweni matano.

Kwa mujibu wa polisi katika eneo hilo, moto ulizuka katika bweni moja alasiri na ukasambaa kwa fujo ukichoma mengine manne.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Kahuro Catherine Ringera, kiini cha moto huo bado kinachunguzwa.

“Tunashuku ama moto ulioanzishwa kiuhuni au hitilafu za umeme. Bado uchunguzi unaendelea. TunaMshukuru Mungu kwa kuwa hakuna aliyejeruhiwa ingawa waathiriwa walipoteza nguo, vitabu, na malazi,” akasema Bi Ringera.

Maafisa wa zimamoto wa kaunti walifika katika shule hiyo na kufanikiwa kuuzima moto huo nao polisi wakiendelea na kuwahoji wadau.

Mabweni yaliyoteketea katika shule ya Kirogo Boys iliyoko Kahuro, Kaunti ya Murang’a. PICHA | MWANGI MUIRURI

Shule hiyo imekuwa na historia mbovu ya moto kuzuka katika hali za utovu wa kinidhamu.

Bi Ringera aliwahakikishia wazazi kwamba hali iko shwari huku wasimamizi wa shule hiyo wakisema watatoa mwelekeo wa iwapo wanafunzi watatumwa nyumbani wakingojea ukarabati au watahifadhiwa katika maeneo mbadala.

Wazazi waliokuwa wameingiwa na wasiwasi walikuwa wakipiga simu kwa vyombo vya habari wakitaka habari zaidi kuhusu athari za moto huo.

Hata hivyo, walimu walidhibiti hali kupitia kutoa habari kwa simu za mkononi za wazazi na pia kuweka maelezo zaidi katika mitandao ya kijamii ambayo huwaleta pamoja wazazi na wadau muhimu wa shule hiyo.

[email protected]