Habari Mseto

Moto wa karatasi wateketeza kiwanda cha gesi

February 4th, 2019 1 min read

NA LAWRENCE ONGARO

WAWEKEZAJI wa kiwanda kimoja mjini Thika wanakadiria hasara baada ya mali yao kuchomeka kutokana na moto wa karatasi.

Kiwanda cha Africa Alternative Energy System Ltd, kinachotengeneza gesi ya kupikia na mafuta ya Dizeli  kilichomeka Jumamosi mchana na kuwachukua wazima moto saa mbili kuzima ndimi za moto huo.

Iliwalazimu maafisa wa idara ya kuzima moto ya Kaunti ya Kiambu kusafirisha magari matatu ya kuzima moto ili kukabiliana na moto huo uliochoma kiwanda kutoka upande wa nje.

Takataka hiyo iliyochanganyika na mafuta ya dizeli ilidaiwa kuzua moto baada ya kukisiwa kuna mtu aliwasha kiberiti.

Taifa Leo Dijitali ilipofika eneo hilo, ilipata wafanyakazi wakiwa wamesimama nje ya kiwanda hicho huku wazimamoto wakiwa katika harakati ya kuuzima.

Meneja mmoja wa kiwanda hicho Bw Anthony Safari, alisema moto huo ulitokea ghafla ambapo bado wanafanya uchunguzi kubaini aliyewasha kiberiti hicho.

“Tunafanya uchunguzi ili kujua chanzo halisi cha moto huo,” alisema Bw Safari.

Hata hivyo wakazi wa kijiji cha Kiganjo waliohojiwa walisema kiwanda hicho kimewaathiri sana kutokana na gesi mbaya inayotoka huko.

“Sisi kama wakazi wa eneo hili tungeomba serikali ituondolee kiwanda hiki kutoka hapa. Ifikapo usiku sisi hatupati usingizi .Kiwanda hicho hutoa moshi mbaya ambayo imetuathiri afya zetu,” alisema Bw Joshua Mungai ambaye ni mkazi wa Kiganjo.

Alisema watoto wao wengi huathiriwa na homa ya mapafu, kukohoa na hata athma.

Naye mkazi mwingine James Mburu alisema kiwanda hicho kinatengeneza gesi na dizeli ambayo inaathiri sana afya ya binadamu.

“Hata kuna shule moja karibu na kiwanda hicho ambalo lina wanafunzi walioathirika na maradhi ya kifua na kuathirika ngozi,” alisema Bw Mungai.