Moto waangamiza watoto 10 wachanga hospitalini Senegal

Moto waangamiza watoto 10 wachanga hospitalini Senegal

NA MASHIRIKA

DAKAR, SENEGAL

WATOTO kumi wachanga Alhamisi walifariki kwenye moto mkubwa uliotokea katika hospitali moja, mjini Tivaouane, nchini Senegal, alisema rais wa taifa hilo, Macky Sall.

Kulingana na ripoti zilizotolewa, moto huo ulitokea katika eneo ambalo wanawake huwa wanajifungulia watoto.

Ripoti za awali zilisema kuwa moto huo ulisababishwa na hitilafu za umeme.

Meya wa mji huo, Demba Diop, alisema kuwa watoto watatu walifanikiwa kuokolewa kutoka kwa moto huo.

Meya huyo alisema kuwa moto huo ulisambaa haraka, hali iliyofanya shughuli za uokozi kuwa ngumu na kuathirika pakubwa. Hospitali hiyo ilizinduliwa majuzi baada ya ujenzi wake kukamilika.

“Ninatoa rambirambi zangu kwa mama za watoto hao na familia zao,” akasema Rais Sall kwenye taarifa.

“Hili ni tukio chungu na la kusikitisha sana,” akasema Waziri wa Afya Abdoulaye Diouf, ambaye yuko jijini Geneva, Uswisi, anakohudhuria mkutano ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema kuwa uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha mkasa huo. Alisema atakatisha ziara yake kurejea nchini humo mara moja.

Kisa hicho kimezua hisia kali katika mitandao ya kijamii, kuhusu vile taifa hilo lilivyojitayarisha kukabili mikasa katika hospitali za umma.

“Watoto wengine wachomekea katika hospitali za umma. Hili halikubaliki,” akasema mbunge Mamadou Lamine.

Shirika la Amnesty International liliirai serikali ya taifa hilo kubuni jopo maalum kubaini wahusika wakuu.

“Ni lazima serikali ibuni jopo huru la uchunguzi kubaini wale waliohusika na kuhakikisha wamechukuliwa hatua za kisheria,” akasema mkurugenzi wa shirika hilo nchini humo, Seydi Gassama.

Shirika liliitaka serikali kukagua hali ya usalama katika wadi zote za akina mama kujifungulia watoto, baada ya kisa kingine kama hicho kufanyika katika mji wa Linguere mwaka 2021.

Kwenye kisa hicho, watoto wanne wachanga walifariki baada ya moto mkubwa kutokea katika wadi ambazo wanawake huwa wanajifungulia.

Meya wa mji huo alisema kisa hicho kilitokana na tatizo la umeme katika wadi hiyo.

Kisa cha Alhamisi kinafuatia mkasa mwingine, ambapo mwanamke aliyekuwa karibu kujifungua alifariki huku akiwaomba madaktari kumfanyia upasuaji ili kumwezesha kujifungua.

Inaelezwa mwanamke huyo alifariki baada ya kungoja upasuaji huo kwa karibu saa 20. Mtoto wake pia alifariki.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa zaidi ya watu 80,000 wanahitaji msaada wa chakula kwa dharura nchini DRC Congo, baada ya kuachwa bila makao kutokana na mapigano yanayoendelea.

Mapigano kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa kundi la M23 yameongezeka sana katika siku za hivi karibuni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Wale ambao wametoroka makwao wamejificha katika makanisa na shule, kulingana na Afisi ya Umoja wa Mataifa ya Kushughulikia Masuala ya Kibinadamu (OCHA).Mashirika ya kibinadamu yalisema “kuna uwezekano mzozo huo ukaWA mbaya zaidi.”

Kwenye taarifa Jumatano, msemaji wa gavana wa mkoa huo alisema “wanakabiliwa na hali ya kusikitisha sana.”“Tunawaomba wenyeji kuzingatia utulivu japo kuwa wenye tahadhari,” akasema Jenerali Sylvain Ekenge.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Gareth Southgate aita Jarrod Bowen na James Justin...

Karua atoa ahadi ya kuzidi kutetea wanawake wote

T L