Habari Mseto

Moto waharibu vibanda kadhaa sokoni Gikomba

February 1st, 2020 1 min read

 

Na ELVIS ONDIEKI

VIBANDA kadhaa vimeharibiwa Jumamosi na moto katika sehemu ya Jua Kali ya soko maarufu la Gikomba, Nairobi.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kupitia chapisho katika ukurasa wa mtandao wa Twitter kwamba timu za uokozi zimefika eneo la mkasa.

Wazimaji moto wamekabiliana na mkasa huo huku wafanyabiashara wakitafuta chochote kilichosalia.

Mnamo Juni 2018, soko hilo lilishuhudia tukio baya zaidi katika miaka ya hivi karibuni ambapo moto uliangamiza maisha ya watu 15.

Katika miaka ya hivi punde, wafanyabiashara katika soko la Gikomba wamekuwa wakishuhudia hasara kubwa kufuatia matukio ya moto yanayoangamiza biashara zao.

Hali hiyo ilimchochea Rais Uhuru Kenyatta mnamo Oktoba 6, 2017, kuagiza polisi wachunguze kiini cha moto ulioharibu mali yenye thamani ya mamilioni katika soko hilo, tukio lingine lilipotokea.

“Tukio hili limewaathiri wafanyabiashara wengi kutoka kote nchini na uchunguzi unastahili kuzinduliwa kutafuta washukiwa na hatua kuchukuliwa dhidi yao,” Rais alisema wakati huo akiwa anasaka kura katika Kaunti ya Meru katika uwanja wa Maua, Meru.