Habari

Moto wateketeza bweni wanafunzi UoN wakilalamikia kifo cha mwenzao

March 10th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), bewa kuu, Jumatatu jioni walizua fujo na kuteketeza bweni wakilalamikia kuuawa kwa mwenzao kwa njia tata.

Ilidaiwa kuwa mwanafunzi huyo, aliyetambuliwa kama Kyte Ondeng, alishambuliwa na walinzi wanaolinda mabweni Jumatano wiki jana.

Samuel Ayoma ambaye ni kiongozi wanafunzi aliambia ‘Taifa Leo’ kwamba marehemu alishambuliwa na walinzi hao ambao baadaye walimtelekeza katika uwanja wa Central Park, hatua chache kutoka majengo ya chuo hicho.

“Walinzi hao walidai kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mhalifu ilhali ukweli ni kwamba yeye ni mwenzetu,” akasema Bw Ayoma.

Alieleza kuwa jengo ambalo liliteketezwa na wanafunzi ni bweni ambalo hujulikana kama “prefabs” na huwa halitumiki.

Shughuli za masomo zilivurugwa majira ya jioni baada ya wanafunzi hao kusababisha ghasia.

Wenye magari walilazimika kukwepa barabara za Mamlaka Road, Nyerere Road na University Way ili wasikutane na wanafunzi hao waliokuwa wakipiga mayowe wakidai haki.

Mwili wa Ondeng’ umehifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Nairobi.