Habari

Moto wateketeza karakana Starehe Boys

February 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MOTO umezuka katika shule maarufu ya Starehe Boys Centre, Nairobi na kuharibu majengo mawili Jumamosi.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, kaimu mkurugenzi wa shule hiyo Josephat Mwaura alisema moto huo ulianza mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni katika karakana kabla ya kuenea katika madarasa.

“Mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni, moshi ulionekana ukifuka kutoka kwa jengo moja ambako kuna karakana. Wanafunzi ambao walikuwa wamesalia shuleni baada ya wenzao kuelekea nyumbani kwa likizo fupi walikuwa wamekongamana wakaguliwe kama ilivyo ada shuleni humu,” akasema.

Bw Mwaura hata hivyo alisema hakuna majeruhi yaliyotokea katika mkasa huo.

“Tulichua hatua za haraka na tukahakikisha kuwa wavulana wetu wote walikuwa salama,” akasema huku akiongeza kuwa zimamoto Kaunti ya Nairobi walifika haraka na kudhibiti moto huo.

Mnamo Februari 6, 2020, moto uliharibu vitanda na mali ya wanafunzi katika Shule ya Upper Hill, Nairobi.

Mwalimu Mkuu Peter Maina alisema hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho na kwamba moto huo ulizimwa haraka.

Mwalimu huyo mkuu hakufichua chanzo cha moto huo lakini akawahakikishia wazazi kwamba watoto wao walikuwa salama.

Mnamo Novemba 2019 mwanafunzi wa kidato cha tatu alifariki bweni liliposhika moto katika Shule ya Upili ya Bahati PCEA, Kaunti ya Nakuru.

Naibu Kamanda wa Polisi Nakuru Kaskazini Francis Mwangi alisema msichana huyo ndiye alikuwa katika bweni hilo moto huo ulipozuka.

Afisa huyo alisema wanafunzi wote wa shule hiyo walisalia salama.