Kimataifa

Moto wateketeza Notre Dame

April 16th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

MOTO mkubwa ulizuka Jumatatu na kuteketeza paa la jumba maarufu la Notre Dame jijini Paris.

Wingu la moshi la kijivu lilionekana kuelekea angani.

Moshi ulionekana kutoka kwenye paa la jumba hilo lenye historia ndefu ambalo mamilioni ya watalii huzuru kujionea.

Msemaji anayesimamia hapo alisema kwamba mbao za paa la jumba hilo ziliteketezwa na moto huo.

Wazima moto walikisia kuwa moto huo huenda ulisababishwa na ukarabati unaoendelea katika jumba hilo.

Kutokana na mkasa huo wa moto, Rais Emmanuel Macron alilazimika kuahirisha hotuba kuu kwa taifa aliofaa kutoa Jumatatu jioni.

Kwenye mtandao wake wa Twitter, Meya wa Paris Anne Hidalgo alitaja mkasa huu kama wa “kutisha mno.”

Sherehe za Pasaka

“Zimamoto wa Paris wanajaribu kuuzima moto huu,” aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter akazidi kuomba wakazi kutosonga karibu na eneo la mkasa.

Malori ya zimamoto yalionekana yakipita kwa kasi kuelekea eneo la Ile de la Cite.

Idara ya polisi wa Paris nayo katika mtandao wa Twitter ilionya wakazi kutosonga karibu na eneo la mkasa na kuwataka wakazi hao “kuacha nafasi ya magari ya kuokoa.”

Rais wa Amerika, Donald Trump kwenye ukurasa wake wa mtandao Twitter alisema: “Inatisha na kushangaza kutazama moto huu mkubwa ukiteketeza Notre Dame Cathedral iliyoko Paris.”

Watu kadhaa walikusanyika wakiona moto ukiangamiza jumba hilo, wengine kati yao wakinasa video na picha kutumia rununu zao, mwanahabari wa AFP alisema.

Imekusanywa na Daniel Ogetta