Habari za Kaunti

Moto wateketeza nyumba 50 Kangemi

May 1st, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MALI ya thamani isiyojulikana imeteketea kwenye moto uliotokea Waruku, Kangemi, Kaunti ya Nairobi. 

Mkasa huo wa moto ulianza jioni na kulingana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Muthangari, Abdikadir Mohammed, zaidi ya nyumba 50 zimeteketea.

Hata hivyo, hakujaripotiwa kisa chochote cha maafa ama majeruhi.

“Nyumba zisizopungua 50 zinakadiriwa kuchomeka katika kijiji cha Waruku, eneo la Kangemi kufuatia moto uliotokea jioni ya leo (Jumatano),” Bw Mohammed akathibitishia Taifa Leo kwa njia ya simu.

Kikosi cha zimamoto tayari kimefika katika eneo hilo ili kuuzima moto huo na kuuzuia kusambaa zaidi.

“Kufikia sasa, hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa,” akasema Bw Mohammed.

Kwenye video iliyorekodiwa na watu wa kwanza kushuhudia moto huo, wakazi wanaonekana wakihofia usalama wao.

Baadhi ya watu wanasikika wakipiga kamsa.

Chanzo cha moto huo, hata hivyo, hakijabainika.

Taifa Leo inaendelea kufuatilia kinachojiri katika eneo hilo.