Habari za Kitaifa

Polisi Kilifi wachunguza chanzo cha moto kwa ofisi za ‘kanjo’

June 4th, 2024 1 min read

NA MAUREEN ONGALA

POLISI mjini Kilifi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa cha moto ulioteketeza ofisi za serikali ya Kaunti ya Kilifi katika mji wa Kilifi mnamo Jumatatu jioni.

Mkuu wa Polisi wa Kilifi Kaskazini Bw Kenneth Maina, alisema mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa wakati wa kisa cha moto huo.

“Kulikuwa na kisa cha moto Jumatatu saa kumi na mbili jioni katika jengo ambalo kwa kawaida huwa ni la askari wa kaunti almaarufu kanjo. Hatuwezi kubaini chanzo cha moto huo lakini tumeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema Bw Maina.

Alisema hakuna kifo au majeraha yoyote yaliyoripotiwa wakati wa mkasa huo.

Moto huo katika ofisi za askari wa kaunti ulienea katika vyumba vyenye rekodi muhimu za serikali ya kaunti.

Hata hivyo, maafisa wa zimamoto walifika saa mbili na kuanza kupambana na moto huo.

Lakini waliishiwa na maji licha ya kufika hapo na lori la maji.

Gari la zimamoto lililazimika kuendea maji zaidi huku moto ukiendelea kuramba stakabadhi.

Maafisa hao walishindwa kuuzima kabisa moto huo.

Kufikia Jumanne asubuhi, ndimi za moto zilikuwa bado zikionekana ndani ya jengo hilo, ishara tosha kwamba stakabadhi zilikuwa zimevurugika kabisa.

Stakabadhi muhimu zilizoharibiwa na moto mjini Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Wakazi na maafisa walionekana hapo wakiwa wamelemewa na cha kufanya.

Miongoni mwa stakabadhi zilizoteketea ni za Idara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi ambayo ofisi zake ziko kwenye jengo la Hazina ya Kaunti linalofanyiwa ukarabati.

Stakabadhi nyingine zilikuwa fomu za Hazina ya Mfuko wa Basari za Masomo za Wadi ya Kilifi, na risiti za malipo za idara ya maji.

Jengo lililoteketea pia hutumika kama ofisi za manispaa ya mji wa Kilifi.