Habari

Moto wateketeza soko la Toi, maswali mazito yaibuka

March 12th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

MALI ya thamani ya mamilioni ya fedha iliteketea jana katika Soko la Toi mtaani Kibera, Nairobi huku kinara wa Upinzani Raila Odinga akidai kuwa lsoko hilo lilichomwa na wanyakuzi wa ardhi.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Nairobi Philip Ndolo chanzo cha moto huo bado hakijulikani lakini uchunguzi unaendelea.

Bw Odinga aliyekuwa akihutubia waathiriwa Jumanne katika eneo la mkasa amesema serikali na upinzani hawataruhusu Soko la Toi kunyakuliwa na mabwanyenye huku wafanyabiashara zaidi ya 5,000 wanaotegemea soko hilo wakihangaika.

Moto huo ulianza majira ya saa tisa alfajiri  katika moja ya vibanda na kusambaa katika vibanda vingine zaidi ya 1,900.

“Kwanza nimesema pole, hii si mara ya kwanza Soko la Toi kuteketezwa. Soko hili limechomwa kimakusudi,” amesema Bw Odinga aliyekuwa ameandamana na baadhi ya wabunge wa ODM.

“Sasa kuna wale wanyakuzi ambao wakiona kiwanja popote wanaenda wananyakua. Nina hakika hao ndio wamefanya hii njama ya kuteketeza halafu kesho waje na askari hapa waanze kujenga. Nataka kuwaambia ng’oo!” akaongezea.

Bw Odinga amemtaka Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuzungusha ua wa mabati katika soko hilo na kuwajengea wafanyabiashara vibanda vipya.

“Hatuwezi kukubali watu wetu kuhangaishwa kutolewa kama mbwa pale wanapata riziki yao. Hatutaweza kukubali yeyote aingie hapa,” akasema Bw Odinga.

Balozi wa Miundomsingi wa Umoja wa Afrika (AU) amesema kuwa hivi karibuni yeye na Rais Uhuru Kenyatta watazuru eneo la Kibera kuzindua miradi ya maendeleo.

“Sisi tuna mpango wa kuleta mradi mkubwa hapa Kibra ya kuboresha hali ya maisha hapa na karibuni mimi na Rais Uhuru Kenyatta tutakuja hapa tuzindua ujenzi wa mradi huo.

“Tayari tumeweka kamati ya kuzungumza na jamii inayoishi hapa ili tujue tutakavyofanya huo mpango,” akasema Bw Odinga.

Kukarabati

Gavana Sonko amesema Sh5 milioni zimetengwa kwa ajili ya kujenga upya soko hilo ambalo limejizolea umaarufu kwa kuuza mitumba, viatu na bidhaa nyinginezo kwa bei nafuu.

Wafanyabiashara, hata hivyo, walilaumu zimamoto wa Kaunti ya Nairobi kwa kujikokota kufika katika eneo la mkasa.

“Zimamoto wa Kaunti ya Nairobi waliitwa mara tu baada ya moto huo kutokea lakini hawakuwa na maji. Gari lililokuwa na maji liliwasili huku mamia ya vibanda vikiwa tayari vimeteketezwa,” akasema Bw Albert Njoroge, mfanyabiashara katika soko hilo.

Mwaka 2018 soko la Toi liliteketezwa huku wafanyabiashara wakielezea hofu yao kuwa watu wenye ushawishi serikalini walitaka kunyakuwa kipande hicho cha ardhi.

Soko maarufu la Gikomba jijini pia limekuwa likiteketezwa mara kwa mara na kufikia sasa polisi hawajafichua kiini cha mikasa hiyo licha ya kuwepo kwa uvumi kwamba mioto hiyo inaschochewa na ushindani wa kibiashara.