Kimataifa

Motoni kwa kuua mtoto aliyeshindwa kukariri vifungu vya Biblia

February 6th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WANANDOA wamekamatwa kuhusiana na kisa ambapo mtoto wao wa miaka saba alifariki, ikihofiwa kuwa walimuadhibu kwa kukosa kuelewa vifungu vya Biblia.

Timothy na Tina Hauschultz (pichani), pamoja na mtoto wao wa miaka 15 wanadaiwa kumuadhibu mtoto huyo kwa jina Ethan kubeba mzigo mzito kwa muda mrefu kila siku kwa wiki moja, huku kakake akisemekana kumpiga mtoto huyo mateke na mangumi zaidi ya mara 100, pamoja na mateso mengine.

Baadaye, mtoto huyo anadaiwa kuwa alizikwa katika jeneza la barafu akiwa hai, shirika moja la habari likaripoti.

Aliaga dunia mnamo Aprili 2018 na ripoti ya daktari ilionyesha kuwa mtoto huyo alifariki kutokana na mateso na kupigwa kichwani, mgongoni, kifuani na kwenye mbavu.

Baba na tineja huyo wameshtakiwa kwa mauaji na kushirikiana kutekeleza mauaji, naye mama akishtakiwa kwa kutozuia mtoto kujeruhiwa.

Tineja huyo alieleza polisi kuwa alikuwa akiwaadhibu watoto wawili kwa kushindwa kukariri vifungu 13 vya Biblia ambavyo Timothy, baba, aliwataka.

Mamake mtoto huyo alizungumza baada ya mwanawe kufariki, akisema alifika kama tayari ameaga dunia.

“Tulijaribu kumrejesha uhai kwa saa tano lakini hatukuhisi mpigo wa moyo, alikuwa tayari amekufa,” akasema mama huyo kwa jina Tina, wa miaka 35.

Lakini alisema kuwa anataka haki itekelezwe kwa mtoto wake, akisema aliyemuua anafaa kwenda jela.