Habari Mseto

Motoni kwa ulaghai wa kununua nguo

August 15th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumanne kwa kupokea Sh6.7 milioni akijifanya alikuwa na uwezo wa kumsaidia mmiliki wa maduka jijini Nairobi kununua Kontena ya nguo za kuvaliwa na wanaume kutoka bandari ya Mombasa.

Wakili wa Serikali Bi Kajuju Kirimi alimweleza hakimu mkuu katika mahakama ya Nairobi Bw  Francis Andayi kuwa mlalamishi Bi Flora Kisale, alidanganywa atanunuliwa mavazi hayo wanaume katika mnada unaofanywa kwenye bandari ya KPA  kaunti ya Mombasa.

Bi Kirimi aliongeza kueleza hakimu kuwa mshtakiwa, Bw Maurice Ouma Opiyo, hakuwa katika hali ya kuweza kununua nguo hizo katika mnada huo unaofanywa katika bandari ya KPA.

Mshtakiwa alikanusha shtaka kuwa alipokea Sh6,700,000 kutoka kwa Bi Kisale kati ya Julai 27 na Agosti 2 mwaka huu kati kati mwa jiji la Nairobi.

Bw Opiyo aliomba aachiliwe kwa dhamana .

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana. Mimi ni raia wa nchi hii na sina rekodi ya uhalifu ya hapo awali,” Bw Opiyo alimsihi hakimu

Mshtakiwa aliambia korti atatii masharti atakayopewa na kuhakikisha amefika kortini siku za kusikizwa kwa kesi dhidi yake.

Mshtakiwa alieleza korti  kuwa ameoa na familia yake inayojumuisha mke na watoto inamtegemea kujikimu kimaisha.

“Siwezi kukosa kufika kortini. Ninafanyakazi jijini Nairobi na kamwe siwezi toroka,” Bw Opiyo alieleza korti.

Pia aliomba korti iamuru apewe nakala za mashahidi na stakabadhi zozote ambazo  upande wa mashtaka utategemea kuwasilisha kortini.

“Nahitaji nakala za mashahidi niandae utetezi wangu. Naomba korti iamuru upande wa mashtaka,” mshtakiwa alirai.

Bi Kirimi alimweleza hakimu , “ hajapata maagizo yoyote apinge mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.”

Akitoa uamuzi , Bw Andayi aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 kabla ya kuachiliwa kutoka korokoroni.

Pia aliamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala za ushahidi na stakabadhi zile zitakazotegemewa kama ushahidi.

Kesi hiyo imeorodhesha kusikizwa Septemba 3, 2018.