Habari Mseto

Motoni kwa ulanguzi wa wasichana kutoka Burundi

April 24th, 2018 1 min read

Mzee Kasso Abdalla (kulia) na Bigirumana Hassa, raia wa Burudi wakiwa kizimbani kwa ulanguzi wa wasichana. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MKENYA pamoja na raia wa Burundi walishtakiwa Jumatatu kwa ulanguzi wa binadamu.

Mzee Kasso Abdalla Ebrahim mwenye umri wa miaka 70 na Bw Bigirumana Hassan mwenye umri wa miaka 37 walifikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Nairobi Milimani wakikabiliwa na mashtaka matano ya ulanguzi wa binadamu.

Mabw Ebrahim na Hassan walikanusha mashtaka ya kuwaingiza humu nchini wasichana watano raia wa Burundi wakiwa na lengo la kuwapeleka mataifa ya kigeni.

Walikanusha shtaka la kuwaingiza wasichana hao ambao polisi waliwatambua kwa majina ya herufi zao  V.M, S.K, N.C, N.A na N.B.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alisema wasichana hawa waliingizwa humu nchini kupitia njia za mkato na kuzuiliwa katika mtaa wa Ngara.

Bw Naulikha alimweleza hakimu mkuu Bw Francis Andayi kwamba polisi waliwatia nguvuni washtakiwa hawa wawili pamoja na wasichana hao waliokuwa wanalanguliwa.

“ Walalamishi hao watano wanazuiliwa katika hifadhi maalum ndipo wafike mbele ya hii mahakama kutoas ushahidi,” alisema Bw Naulikha.

Korti ilifahamishwa zaidi kuwa washtakiwa hawa walikuwa wanawazuilia walalamishi hao kinyume cha sheria wakiwa na lengo la kuwauzia mabwanyenye kuwapelekaq nchini Dubai kufanya kazi za ujakazi nchi humo.

Washtakiwa hao waliomba waachiliwe kwa dhamana wakisema “ni haki yetu.”

Mahakama ilielezwa washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana kuna uwezekano wao kutoroka.

Bw Andayi aliwaamuru walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh2milioni. Kesi imeorodheshwa kusikizwa Mei 16, 2018.