Michezo

Mount Kenya United utovu wa nidhamu umezidi – takwimu

March 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MOUNT Kenya United ndiyo klabu yenye utovu mkubwa wa nidhamu kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Kenya nayo Vihiga United inaongoza katika kudumisha nidhamu, takwimu za kadi zilizotolewa Alhamisi na kampuni inayoendesha ligi hiyo ya klabu 18 inaonyesha.

Kwa mujibu wa takwimu za KPL, Mount Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya 16 ligini, imeonyeshwa kadi 24 za njano, mbili za njano kwa mara ya pili mechini na mbili nyekundu za moja kwa moja.

Nambari sita ligini Kariobangi Sharks ni ya pili katika kukosa nidhamu baada ya kujizolea kadi 26 za njano na mbili nyekundu za moja kwa moja.

Wanajeshi wa Ulinzi Stars wanashikilia nafasi ya tatu katika utovu wa nidhamu.

Ulinzi, ambayo inafunga 10-bora ligini, imelishwa kadi 29 za njano na moja nyekundu ya moja kwa moja. Sofapaka imeshuhudia wachezaji wake wakilishwa kadi ya njano mara 30 na kupokea kadi mbili za njano mara moja bila kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mabingwa hawa wa Kenya mwaka 2009 wanashikilia nafasi ya tano ligini. Nambari 11 ligini Nzoia Sugar imepokea kadi 25 za njano na mbili nyekundu za moja kwa moja. AFC Leopards, ambayo iko mkiani ligini, haijawachwa nyuma katika utovu wa nidhamu.

Baadhi ya wachezaji wa Mount Kenya United washerehekea bao la Peter Amani katika mchuano na timu mojawapo ya ligi kuu nchini Kenya. Picha/ Maktaba

Inashikilia nafasi ya sita katika kukosa nidhamu baada ya kuonyeshwa kadi 29 za njano na moja nyekundu ya moja kwa moja. Viongozi wa ligi Bandari wanafuata Leopards kwa kupokea kadi 27 za njano na moja nyekundu ya moja kwa moja.

Mabingwa watetezi Gor Mahia wamelishwa kadi 22 za njano na mbili nyekundu ikiwemo moja dhidi ya Tusker mnamo Februari 27 katika mechi ambayo vijana wa Hassan Oktay walishinda 1-0 na kurukia nafasi ya pili ligini.

Vihiga iko pabaya

Vihiga, ambayo inakodolea macho kutemwa kutoka Ligi Kuu kwa kushikilia nafasi ya 17, imeonyesha nidhamu ya hali ya juu kuliko wote kwa kupokea kadi 10 za njano bila adhabu nyingine yoyote ya kadi. Inafuatiwa katika nafasi ya pili na SoNy Sugar ambayo imelishwa kadi 17 za njano na moja nyekundu.

Kakamega Homeboyz ni ya tatu kwa kadi 22 za njano. Western Stima ni nambari nane ligini na nne katika nidhamu baada ya kuonyeshwa kadi 23 za njano nayo nambari 13 ligini Posta Rangers inafunga mduara wa tano-bora kwa kadi 20 za njano na moja nyekundu ya moja kwa moja.

Nambari tatu ligini Mathare United ni ya sita kwa kadi 21 za njano na moja nyekundu nayo Zoo imelishwa kadi 19 za njano, moja ya njano kwa mara ya pili na moja nyekundu ya moja kwa moja.

Zoo inashikilia nafasi ya 15 ligini na saba kwenye nidhamu. Tusker na Chemeli, ambazo ligini ni nambari nne na 14 mtawalia, zinapatikana katika nafasi ya nane na tisa katika nidhamu baada ya kula kadi 25 za njano kila moja.

KCB inafunga mduara wa 10-bora katika nidhamu kwa kadi 23 za njano, moja ya njano kwa mara ya pili na moja nyekundu. Inashikilia nafasi ya 12 ligini.