Michezo

Mount Kenya University FC inavyotesa wapinzani ligini

September 15th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Klabu ya Mount Kenya University FC inayoshiriki ligi ya divisheni ya pili FKF kaunti ya Nakuru, inajivunia huduma za wachezaji mahiri wanaovumisha jina ya timu.

Ikiwa miongoni mwa vikosi vinavyofanya vizuri katika ligi ya FKF divisheni ya pili ukanda wa kati, tawi la Magharibi inatumia zana hatari kulemaza wapinzani.

Licha ya Changamoto nyingi wachezaji wengi hapa hawajaonekana kukata tamaa wala kuyumbishwa, kutokana na ukosefu wa ufadhili jambo linalowafanya vijana wengi kuachana na soko.

Wengi wao wakitafuta vilabu vya mataifa ya ulaya, kutokana na miundo misingi duni na utepetevu kutoka kwa idara inayosimamia jumuia ya michezo kwa chipukizi.

Mmoja wao ni Felix Omondi ambaye msimu uliopita na msimu huu amechangia mafanikio ya Mount Kenya kwa asilimia kubwa jambo lililomfanya kubatizwa jina Messi.wa Kenya.

Anasema hamasa yake inatokana na juhudi za usimamizi wa Chuo cha Mt Kenya tawi la Nakuru kuwapatia wachezaji mwamko mpya katika ulingo wa soka

Aidha anasema ushirikiano na wachezaji wenzake umemsaidia kujiimarishia ujuzi uwanjani unaomsaidia kupakua mipira kwa ustadi,hususan akiwa nje ya kisanduku.

Felix anakumbukwa kwa kuchangia ufungaji wa magoli muhimu kwenye michuano ya shirikisho,kutokana na uzoefu wake kila anapotua uwanjani,kupambana na timu hasimu.

Mchango wake umemfanya kuamini kuwa siku moja ataisaidia timu ya taifa Harambe Stars kunyakua kombe la mataifa bingwa barani Afrika,na kuwakilisha nchi katika kombe la dunia.

Ndoto yake ni kuichezea timu ya Kariobangi Sharks ,na hivi karibuni anaona kuwa matarajio yake yataishia kuzaa matundaa ili aweze kudumu kwenye mchezo wa soka.

“Nitapata nafasi nzuri kujitangaza kwa timu zinazoshiriki michuano ya ligi ya kitaifa KPL na kwa timu za bara uropa,”akasema Felix ambaye hucheza nambari 6,8 au 10.

Edward Kwintira akiwapatia wachezaji wake masharti wakati wa mazoezi. Picha/ Richard Maosi

Felix anasema anafurahia kuichezea timu ya Mount Kenya akiwa miongoni mwa nguzo muhimu za kutegemewa,akisema mazoezi ya kila mara yamemweka pazuri.

Aidha anafuata nyayo za wachezaji mahiri kama vile Paul Pogba ambaye anaichezea timu ya Manchester United inayoshiriki ligi ya EPL nchini Uingereza.

Kulingana na kiungo huyu aliisaidia timu yake kucharaza Bigot FC,Nakuru All Stars,Ravine Roses na Geothermal Development Cooperation (GDC) ,timu zenye ushindani mkali ligini.

Mchango wake ukiwa ni kulinda ngome na kuisadia timu ya mashambulizi kutekeleza maangazizi kwa kufunga magoli mengi,awamu hii wanaposaka nafasi ya kuwa miongoni mwa timu tatu bora.

Felix anasema safari yake katika taaluma ya soka ilianza mnamo 2015 akiwajibikia timu ya Lambwe katika kaunti ya Homabay,ambapo kabumbu safi ilivutia timu kutoka bonde la ufa

Kisha akagura hadi kwenye kaunti ya Nakuru ambapo aliichezea timu ya Egerton kabla ya kuviziwa na Langalanga FC inayoshiriki ligi ya kaunti ya Nakuru ukanda wa kati ,tawi la Magharibi.

Kabla ya hapo aliwahi kuichezea timu ya Mbita United ambapo mchango wake uliisaidia kunyakuwa taji la kaunti mara mbili mtawalia ,na kuweka rekodi ambayo bado imesimama.

Mkufunzi Edward Kwintira anasema ni kijana mwenye maono ambaye siku moja atakuja kushangaza ulimwengu wa soka muradi atajiongezea tajriba,Ndio maana anawashauri wachezaji wake kushiriki mechi nyingi za kirafiki ili kujipima nguvu.

Felix Omondi (kushoto) akipambana na mabeki wa tiimu ya Ravine Roses katika mchuano wa ligi ya kaunti ya Nakuru siku ya Jumapili. Picha/ Richard Maosi

Bidii zake na weledi wa kupenya baina ya wapinzani hazina kifani ambapo vilabu kadhaa vinamuwania kama andazi moto.

“Ingawa anasema azma yake ni kucheza soka ya kulipwa kwanza anataka kujitengenezea jina humu nchini kabla ya kuhamia timu nyingine,”akasema.

Felix Omondi anasema itakuwa jambo la manufaa endapo serikali itawekeza katika soka miongoni mwa vijana ili kunoa zana za siku za baadae.

Anaona afadhali vijana wafahamu kuwa kuna njia nyingi za kupata ajira na mojawapo ikiwa ni kutokana na utumiaji wa vipaji kwa njia sahihi.

Felix Omondi mchezaji wa timu ya Mt Kenya FC akifanya mazoezi katika uwanja wa Nakuru Athletics Club. Picha/ Richard Maosi

Aidha anasema ni vyema kama serikali ya ugatuzi itafuatilia namna hela za wachezaji zitakuwa zikitumika katika juhudi za kuwaimarisha na kuwatengenezea jina katika ulingo wa soka inayozidi kukubwa na utata.

Anawaaomba wachezaji kuwa wazalendo na kujivunia soka ya nchi yao kabla ya kusakatia soka mataifa ya kigeni ambapo miundo msingi ni bora.

Pia anawahimiza vijana chipukizi wanaojaribu kuibukia katika ulingo wa soka kujitenga na utumiaji wa mihadarati na mogoka.