Michezo

Mourinho aapa kuiadhibu Juventus UEFA

October 23rd, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Jose Mourinho ameahidi kwamba kikosi chake kitaiangushia mibabe wa ligi ya Serie A Juventus ghadhabu zote walizopata katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Chelsea timu hizo zitakapokutana katika mechi ya Klabu Bingwa barani Uropa (UEFA) ugani Old Trafford Jumanne Oktoba 23.

Katika mechi dhidi ya Chelsea, Manchester United walikubali bao la dakika ya 96, muda wa ziada na hali tete kuzuka baada ya mojawapo wa makocha wa Chelsea, Marco Ianni kusheherekea bao hilo kwa madaha mbele ya Mourinho ambaye hakusita kumwendelea kumpa kipigo ila akazuiwa na wasimamizi wa mechi. Hata hivyo Ianni alimwendea na kumwomba radhi akijutia kitendo chake.

“Uchezaji wa pamoja tuliodhihirisha katika mechi iliyotukutanisha na Chelsea ulikuwa mzuri ila matokeo yakawa vinginevyo. Tutatumia hasira kuwabili Juve na kuwashinda,” akasema Mourinho.

Mkufunzi huyo pia alimsifu nyota wa Juventus Cristiano Ronaldo na kusema kwamba walikuwa na uhusiano mzuri wakati walipokuwa pamoja katika klabu ya Real Madrid, ambao ni bingwa mtetezi wa kipute hicho.

“Cristiano ni moja wa wachezaji wazuri zaidi ulimwenguni na hutaji kuzungumzia mengi kumhusu. Kando na Ronaldo vile vile wanajivunia huduma za wanasoka hodari kama Bonucci, Cancelo na Emre Can,” akaongeza Mourinho.