Michezo

Mourinho alipwa Sh2 bilioni, ajituliza kuchanganua mechi sasa

January 10th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

JOSE Mourinho amepokea fidia yote ya kuachishwa kazi mapema na Manchester United ya Sh1, 947,344,017 na yuko huru kuwa kocha wa klabu nyingine, ripoti zimesema Alhamisi.

Tovuti ya tovuti ya RT inasema kwamba ni rasmi sasa Mourinho hana kandarasi yoyote na United baada ya kupokea kitita hicho cha fedha ambacho yeye na mabingwa hawa mara 20 wa Uingereza walikuwa wamekubaliana akifutwa kazi kabla haijafika mwisho.

Mreno Mourinho, ambaye amepata kitulizo katika kuchanganua mechi za Kombe la Bara Asia zinazoendelea nchini Qatar katika runinga ya beIN Sport, alitemwa Desemba 18, 2018 baada ya kuandikisha matokeo duni katika nusu ya kwanza ya msimu 2018-2019 na pia ripoti kusema amekosana na wachezaji kadhaa muhimu akiwemo kiungo Paul Pogba.

Hata hivyo, tovuti hii inasema kwamba wandani wa karibu wa kocha huyu wa zamani wa Chelsea, Inter Milan na Real Madrid wameieleza kwamba sasa yuko huru kufunza klabu yoyote baada ya kupokea fidia yake yote.

Inasemekana kwamba Mourinho tayari ameambia miamba wa Ureno, Benfica, hayuko tayari kuinoa, huku Madrid ikiaminika kuwa na hamu ya kumuajiri tena.